Wednesday, December 6, 2017

Chadema wasema hawana hofu Kinondoni

 

By Prosper Kaijage, Mwananchi Pkaijage@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Jimbo la Kinondoni kimesema hawana hofu juu ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Maulid Mtulia kuhamia CCM kwani wako imara na kusubiri taratibu za kutangazwa siku ya uchaguzi ili waweze kutetea kiti hicho.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano na mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Kinondoni, Waziri Muhunzi alipokuwa akituma salamu kwa wananchi wa eneo hilo kuwataka kuwa wavumilivu.

"Wananchi wa Jimbo la Kinondoni wako salama kwani Mtulia hakuondoka na wanachama hivyo tuko vizuri na hatujasambaratika kama ilivyodaiwa hapo awali," amesema Muhunzi.

Amesema mbunge wa jimbo hili bado ataendelea kutoka Ukawa licha ya usaliti aliyoufanya Mtulia ili hali Chadema ilipigania kila hatua kuhakikisha amepata nafasi hiyo katika uchaguzi wa 2015.

"CCM hawako salama wasifikiri kumchukua Mtulia wamemaliza Wilaya ya Kinondoni, wanachama wapo na wataendelea kuwepo ndani ya Chadema," amesema.

Kwa upande wake katibu mwenezi Wilaya ya Kinondoni, George Mwingura amesema tangu kuondoka kwa Mtulia hakuna mwanachama aliyetoka kufuatana naye.

-->