Chadema walaani kung’olewa bendera, mabango ya kampeni

Muktasari:

Kampeni meneja wa uchaguzi huo, Charles Chinchibela akiwa kwenye mkutano wa kampeni hizo Uwanja wa Kasota juzi alisema kuwa alipokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu kitendo hicho.

Viongozi wa Chadema mkoani Mwanza, wamelaani kitendo cha baadhi ya watu kung’oa bendera na mabango ya chama hicho yenye mgombea wa udiwani wa Kata ya Mhandu, Godfrey Missane.

Kampeni meneja wa uchaguzi huo, Charles Chinchibela akiwa kwenye mkutano wa kampeni hizo Uwanja wa Kasota juzi alisema kuwa alipokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu kitendo hicho.

“Baada ya kupata taarifa hizo tulifuatilia na kulipata gari hilo likiwa limetelekezwa, ndani yake likiwa na bendera na silaha za jadi kama mapanga na vitu vingine vyenye ncha kali, tulipiga simu polisi na kuja kulichukua kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema Chinchibela.

Hata hivyo, Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Faustine Shilogile alisema hajapata taarifa kuhusiana na tukio hilo.

Alisema ni vyema wanasiasa kufanya siasa zenye tija na kuachana na mambo yasiyofaa kwa kuwa kung’oa bendera na mabango hakupigi kura ila wananchi ndiyo wenye uamuzi wa kuchagua kiongozi bora.

Katibu wa Vijana Chadema (Bavicha) mkoa wa Mwanza, Boniphace Nkobe alisema hawatarajii kampeni hizo kuwa na vurugu licha ya baadhi ya watu wachache kutaka kuziibua.

Mwenyekiti wa wilaya ya Nyamagana, Jafety Nungwana alisema kila mtu ana wajibu wa kufanya siasa za amani na kushindana kwa hoja, siyo kuleta vurugu.