Chadema walaani madiwani wake kukamatwa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha, Aman Golugwa amesema kuwa wanapinga kukamatwa madiwani hao licha ya kupewa dhamana.

Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha kimelaani kukamatwa madiwani wake watatu kwa tuhuma za kutoa siri za kikao cha kamati ya fedha.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha, Aman Golugwa amesema kuwa wanapinga kukamatwa madiwani hao licha ya kupewa dhamana.

Madiwani hao, Naibu meya wa jiji la Arusha, Viola Lindikikok na wenzake wawili, Sabina Francis, Happiness Charles walikamatwa juzi jioni.

Golugwa alisema Viola ndiye mjumbe wa kamati wa kamati ya fedha na anatuhumiwa alirekodi kwa simu kikao jambo ambalo si kweli.

"Polisi walipokuja kumkamata Viola walimkuta na madiwani wenzake ambao walipinga na ndio sababu waliunganishwa wote,"alisema na kuongeza kuwa hata hivyo haijulikani ni nani mlalamikaji katika kesi hiyo.

Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na ukikamilika taarifa zitatolewa.

Meya wa jiji la Arusha, Calist Lazaro akizungumzia tukio hilo alisema kwamba viongozi hao walikamatwa wakiwa ndani ya ofisi yake wakisikiliza kero mbalimbali ikiwa ni siku maalum iliyotengwa kusikiliza kero na kuzitatua.

Alisema ameshangazwa na tukio hilo kwani kama kuna diwani ametoa siri za vikao kuna kamati za maadili za kumhoji na kumwajibisha na si suala la polisi.