VIDEO: Chadema watawanywa kwa mabomu Tarime

Muktasari:

Viongozi wa Chadema akiwamo Esther Matiko wamekamatwa, Zitto Kabwe asema kampeni zitaendelea

Tarime. Mkutano wa kumnadi mgombea udiwani kata ya Turwa, (Chadema) umeshindwa kufanyika baada ya polisi kuwatanya kwa mabomua ya machozi wafuasi wa vyama vya upinzani waliohudhuria mkutano huo.

Wakati huo huo, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na wananchi wengine zaidi ya 10 wamekamatwa na polisi akiwamo mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima, Sita Tuma ambaye pia amekamatwa.

Hata hivyo kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Henry Mwaibambe hakupatikana kuzungumzia kamatakamata hiyo wala simu yake ya mkononi haikupokewa.

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alitarajiwa kuhutubia mkutano huo.

Akizungumzia tukio hilo, katibu wa Chadema mkoa wa Mara, Chacha Heche amedai kwamba chama chake kimezuiwa kufanya mkutano wa kampeni kuanzia leo Agosti 8, 2018 hadi Agosti 11.

Hata hivyo Heche amesema chama hicho hakikupewa barua rasmi ya kuzuiwa kufanya mkutano huu wa kampeni.

“Walikuja asubuhi kwenye ofisi za chama wakitaka tusifanye mkutano lakini hakukuwa na sababu ya msingi ya sisi kutofanya mkutano,” amesema.

Hata hivyo Zitto amesema wataendeleza kampeni hizo kwa kushiriki mikutano ya kampeni ya NCCR-Mageuzi.

Kadhalika Zitto amesema polisi wamemzuia kumuona Esther kituo cha polisi anamoshikiliwa.