Chadema yabadili gia angani

Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe

Muktasari:

Hii ni mara ya pili operesheni hiyo iliyolenga kupinga kile chama hicho ilichodai kuwa ni ukandamizaji wa demokrasia na kuipa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), kuahirishwa kwa sababu mbili tofauti.

Dar es Salaam. Chadema imeahirisha utekelezaji wa operesheni ya Ukuta iliyolenga kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa sababu ilizoita za usalama.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesita kutaja tarehe rasmi ya utekelezaji wa Ukuta, akisema hiyo itasababisha vyombo vya usalama kujipanga kuwadhuru watu wao.

Hii ni mara ya pili operesheni hiyo iliyolenga kupinga kile chama hicho ilichodai kuwa ni ukandamizaji wa demokrasia na kuipa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), kuahirishwa kwa sababu mbili tofauti. Mara ya kwanza ilikuwa kutoa fursa kwa viongozi wa dini kukutana na Rais John Magufuli na sasa kwa sababu za usalama.

Operesheni hiyo iliyotangazwa Julai 27, ilipangwa kufanyika Septemba Mosi lakini ilipingwa na Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Jeshi la Polisi huku Rais John Magufuli akionya kuwa wanaotaka kumjaribu wangekiona cha mtemakuni.