Saturday, August 12, 2017

Chadema yadai Bodi ya Mikopo imekiuka Katiba

Waziri kivuli wa elimu, Suzan Lyimo akizungumza

Waziri kivuli wa elimu, Suzan Lyimo akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis 

By Peter Elias na Damian Ndelwa, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka Serikali kuondoa masharti yaliyowekwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ili kutoa fursa kwa Watanzania wengi kujiunga na elimu ya juu kama hitaji lao la msingi na kwamba kinyume chake ni kukiuka Katiba ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Susan Lyimo aliitaka Serikali ipitie upya vigezo vilivyowekwa kuhusiana na sifa za wanafunzi wanaostahili kupatiwa mikopo na kuvifanyia marekebisho ili kutoa fursa sawa kwa Watanzania kupata haki yao ya kupata elimu hadi pale uwezo wa mtu unapokomea.

Alisema Ibara ya 13(2) ya Katiba inatamka wazi kuwa, “Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano kuweka sharti lolote ambalo ni la kibaguzi ama wa dhahiri au kwa taathira yake.”

Alisisitiza kuwa Kifungu cha nne (4) katika ibara hiyo kinasema; “Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote au katika utekezaji wa kazi au shughuli yoyote ya mamlaka ya nchi.”

Alivitaja vigezo vilivyowekwa na HESLB vinavyotakiwa kufanyiwa marekebisho kuwa ni kile cha saba kinachomtaka mwombaji awe amemaliza kidato cha sita au sifa linganishi miaka mitatu iliyopita na kile cha nane kinachomtaka umri wake usizidi miaka 30.

Kigezo kingine ni kile cha tisa ambacho kinamnyima mwombaji nafasi kama mzazi wake ni mkurugenzi au meneja wa kampuni na cha 10 ambacho kinamnyima nafasi kama mzazi wake ni kiongozi wa umma.

Akijibu hoja hizo za Chadema, Mkurugenzi Mkuu wa HESLB, Abdulrazaq Badru alisema kigezo cha mwanafunzi kumaliza kidato cha sita na umri usiozidi miaka 30 kinalenga kutoa muda kwa mwanafunzi huyo kuweza kulipa mkopo wake kwa wakati.

“Hata Sera ya Elimu ya Tamisemi inasema mwanafunzi akifikisha miaka 25 hawezi kujiunga na shule ya sekondari kwa hiyo ni vitu viwili vinavyokwenda pamoja,” alisema.

Kuhusu waliotajwa kwenye Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, Badru alisema hawatarajiwi kuomba mkopo kwa kuwa unalenga watu wenye vipato vya chini.

“Katika kuandaa hivi vigezo tunazungumza na wadau mbalimbali na kuyagusa makundi tofauti tofauti, natarajia mwaka huu kutoa mkopo kwa wanafunzi 30,000.”

Mbali na kulalamikia HESLB, pia Lyimo aliitaka Serikali kuifumua Sera ya Elimu nchini kwa madai kwamba ina upungufu mkubwa na imeshindwa kutengeneza mazingira ya Taifa la watu wenye maarifa na ujuzi katika kada mbalimbali.

Alisema kuna haja ya kuundwa kwa tume maalumu itakayosimamia suala la elimu nchini ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa ukaribu zaidi.

Lyimo alisema vitabu vingi vya shule za msingi ni vibaya lakini ndiyo vinavyotumika kufundishia wanafunzi. Alisisitiza kwamba Serikali inatakiwa kuviondoa vyote kwenye mzunguko na kuchapisha vitabu vipya vya kiada ili wanafunzi wapate elimu bora.

“Tukitaka kuwa na elimu bora, lazima mfumo mzima wa elimu ubadilishwe. Vichapishwe vitabu sahihi, tuwe na falsafa ya elimu, pia miundombinu ya elimu nchini iboreshwe. Ripoti ya Makwetta ilieleza vizuri sana kuhusu hili lakini wameifungia kabatini,” alisema Lyimo.

Pia Lyimo alipinga msimamo wa Serikali wa kutowapokea wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni na kusema wanatakiwa kupewa fursa ya kuendelea na masomo baada ya kujifungua kwa sababu Katiba ya nchi inatoa fursa kwa mtu yeyote kupata elimu kama haki yake ya msingi.

-->