Breaking News
Tuesday, September 11, 2018

Chadema yagonga mwamba kamati ya maadiliJaji Mary Longway

Jaji Mary Longway 

By Mwandishi wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Taifa, imeitaka Chadema kutekeleza uamuzi wa kamati ya maadili ngazi ya Jimbo la Ukonga kuomba msamaha hadharani kwa kosa   ililotenda.

Uamuzi huo umetolewa leo Septemba 10 na mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji Mary Longway baada ya kikao  cha kamati hiyo kupitia na kujadili rufaa dhidi ya uamuzi wa kamati ya maadili Jimbo la Uchaguzi Ukonga.

Rufaa hiyo iliwasilishwa na Chadema Septemba 5, 2018 ikiitaka kamati hiyo itengue uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Jimbo.

Amesema  kwa mujibu wa vielelezo vilivyoambatishwa katika rufaa  hiyo, kamati ya rufaa imefikia uamuzi kuwa rufaa hiyo imewasilishwa nje ya muda wa saa 48 kinyume na maelekezo ya  kipengele cha 5.7 (b) cha maadili tajwa.

Amesema kwa mujibu wa uamuzi wa kamati ya maadili ngazi ya Jimbo la Ukonga, Chadema imeonywa kuhakikisha kuwa inafuata Kanuni na Taratibu za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 na kutekeleza uamuzi  huo ndani ya saa 48 tangu kutolewa na adhabu hiyo.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ukonga, Jumanne Shauri  Agosti 27, 2018 alipokea malalamiko na kupitia utetezi wa Chadema na kujiridhisha kuwa Chadema kilitumia kiongozi wa dini kumpigia kampeni mgombea wa chama hicho kinyume na kifungu cha 2.2 (k) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.

Msimamizi huyo wa uchaguzi ameongeza kuwa: “Dk  Makongora Mahanga akiwa kiongozi wa Chadema, siku ya kampeni Agosti 25 alitumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli na udhalilishaji dhidi ya mgombea wa CCM, ikiwa pia ni kinyume na kifungu cha 2.2 (k) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.”

Mbali na uamuzi juu ya rufaa hiyo, kamati hiyo pia imepitia barua ya Septemba  5  iliyowasilishwa tume Septemba 7, 2018 kupinga maelekezo ya Kamati ya Maadili Jimbo la Ukonga yaliyokiagiza Chadema kuwasilisha ndani ya saa 48 kuanzia  Septemba 4 vielelezo vilivyothibitishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na wataalamu wa lugha ya Kikurya ili kutoa uamuzi shauri husika.

Jaji Longway amesema baada ya kupitia vielelezo na kujadili barua husika, imeamuliwa kuwa rufaa hiyo imekosa sifa kwa kuwa hakuna uamuzi uliofanywa na Kamati ya Maadili Jimbo la Ukonga.

Kutokana na jambo hilo, Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya Taifa imekielekeza Chadema kuwasilisha vielelezo Kamati ya Maadili ya Jimbo la Ukonga kwa uamuzi kama ilivyoelekezwa na kamati husika

-->