Chadema yajiweka sawa kinyang’anyiro cha 2020

Muktasari:

Wakizungumza mjini Musoma, viongozi na madiwani wa Chadema walisema hawawezi kuongoza halmashauri kwa kutumia ilani ya CCM kwa kuwa kufanya hivyo ni kufifisha uhai wa chama chao.

Musoma. Chadema mkoani Mara imesema itatumia ilani ya chama hicho kuongoza halmashauri zilizo chini yake na siyo ya chama tawala cha CCM.

Wakizungumza mjini Musoma, viongozi na madiwani wa Chadema walisema hawawezi kuongoza halmashauri kwa kutumia ilani ya CCM kwa kuwa kufanya hivyo ni kufifisha uhai wa chama chao.

Viongozi wa Serikali na chama tawala kwa mara kadhaa wamekuwa wakihimiza watendaji wa halmashauri kutekeleza ilani ya CCM kwa maelezo kuwa ndiyo iliyounda Serikali iliyopo madarakani.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tarime, Moses Misiwa alisema ruzuku inayotolewa kutokana na kodi za wananchi kutoka serikalini wataielekeza kutekeleza miradi ya wananchi iliyo kwenye ilani ya Chadema.

Misiwa alisema watatumia misingi ya Katiba na sheria za nchi kuongoza halmashauri tatu kati ya tisa zilizo chini ya Chadema mkoani humo.

“Wenyeviti wa halmashauri kupitia Chadema tunawaelewesha wakuu wa wilaya kutambua kuna ilani ya kitaifa na ya Serikali za Mitaa na sisi madiwani tunapogombea tunanadi sera za vyama vyetu vya siasa,” alisema.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche alisema wameandaa mfumo wa kuwapima madiwani kwenye kata zao na watakaoshindwa kutekeleza ilani hawataruhusiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro 2020.

Alisema chama hicho kimeweka mkakati wa kupita kwenye halmashauri zote zinazoongozwa na vyama vya upinzani ili kusaidia madiwani kutekeleza miradi ya maendeleo na kujenga imani kwa wananchi.