Chadema yalia na bodi ya mikopo kuhusu masharti mapya

Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Susan Lyimo

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesikitishwa na masharti yaliyotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa wanafunzi ambao wataomba kupewa mkopo huo kwa mwaka huu wa 2017/18.

Akizungumza na vyombo vy habari leo Ijumaa, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Susan Lyimo amesema masharti hayo ni mabaya na yatawakosesha vijana wengi fursa ya kupata elimu ya juu.

Lyimo amesema HESLB imekiuka matakwa ya Ibara ya 13 ya Katiba mbayo inaeleza kwamba kila mtu ana fursa ya kupata elimu.

"Chadema tumesikitishwa na masharti yaliyotolewa na HESLB, kwa kiasi kikubwa yatapunguza idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu," amesema Lyimo ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu kupitia chama hicho.

Mbunge huyo amebainisha masharti manne yaliyotolewa na bodi ambayo wanayapinga kuwa ni pamoja na lile linalomtaka muombaji awe amemaliza kidato cha sita au sifa linganishi chini ya miaka mitatu iliyopita.

Masharti mengine ni umri usiozidi miaka 30; waombaji ambao ni mameneja au wakurugenzi kwenye makampuni na waombaji ambao wazazi wao wametajwa kwenye sheria ya maadili ya viongozi wa umma, hawatarajiwi kuomba mkopo.

"Masharti hayo yatawakosesha watu wengi kupata mkopo, wapo ambao walimaliza kidato cha sita wakaamua kufanya kazi kwanza baadaye ndiyo waendelee na masomo. Wengi wao wakati huo wana umri zaidi ya miaka 30. Wapo watu ambao ni wakurugenzi wa vikampuni vyao, wanatuambia nao watoto wao hawatapata mkopo. Hiyo siyo haki kabisa," amesema Lyimo.