VIDEO: Chadema yamtaka Maalim Seif

Tangu kuibuka kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa katika historia ya Chama cha Wananchi (CUF) na hasa baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kutambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kama mwenyekiti wake, wachambuzi wa masuala ya kisiasa walitaja mambo matano ambayo katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa hana budi kuyafanya ili kubaki hai kisiasa.

BY Husssein Issa, Mwananchi hissa@mwananchi.co.tz

IN SUMMARY

  • Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Juni 27 mwaka jana, wachambuzi hao walisema Maalim Seif akitaka kupata urahisi wa kufanya siasa, akubali kuzungumza na mshirika wake huyo wa zamani ambaye anatambulika na taasisi zinazosimamia vyama vya siasa nchini au ahamie katika chama kingine cha siasa au aanzishe chama kingine cha siasa na kuachana na CUF au aende mahakamani, lakini pia wakashauri kwamba anaweza kuachana na siasa na kufanya mambo mengine.

Advertisement

Dar es Salaam. Tangu kuibuka kwa mgogoro mkubwa wa kisiasa katika historia ya Chama cha Wananchi (CUF) na hasa baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kutambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kama mwenyekiti wake, wachambuzi wa masuala ya kisiasa walitaja mambo matano ambayo katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa hana budi kuyafanya ili kubaki hai kisiasa.

Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Juni 27 mwaka jana, wachambuzi hao walisema Maalim Seif akitaka kupata urahisi wa kufanya siasa, akubali kuzungumza na mshirika wake huyo wa zamani ambaye anatambulika na taasisi zinazosimamia vyama vya siasa nchini au ahamie katika chama kingine cha siasa au aanzishe chama kingine cha siasa na kuachana na CUF au aende mahakamani, lakini pia wakashauri kwamba anaweza kuachana na siasa na kufanya mambo mengine.

Pengine kwa kutambua hali hiyo ngumu aliyonayo Maalim Seif, jana, Baraza la Wazee la Chadema lilifungua milango kwa kiongozi huyo kujiunga na chama hicho na kwamba kipo tayari kumsimasha kuwania urais wa Zanzibar mwaka 2020.

CUF imedumu kwenye mgogoro wa ndani tangu Agosti, 2015 baada ya Profesa Lipumba kutangaza kujiuzulu uenyekiti ikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu. Juni 13, 2016, alitangaza kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na licha ya mkutano mkuu kuikubali barua yake ya kujiuzulu na kurejea kwenye nafasi yake, jambo lililosababisha mgogoro ndani ya chama hicho.

Mgogoro huo uliongezeka zaidi baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuweka wazi kwamba anamtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti wa chama hicho licha ya kuwapo kwa mgogoro huo.

Hali iliendelea kuwa mbaya zaidi baada ya pande hizo kugawana majengo ya ofisi, upande wa Profesa Lipumba ukishikilia zilizopo Tanzania Bara wakati upande wa Maalim Seif ukishikilia ofisi za Zanzibar.

Juni 4, wabunge 40 wa CUF wanaomuunga mkono Maalim Seif walifungua ofisi yao ya wabunge jijini Dar es Salaam na kutenga chumba kimoja kwa ajili ya kiongozi huyo ili aweze kutekeleza majukumu yake akiwa Tanzania Bara.

Kutokana na mazingira hayo ya kisiasa wachambuzi walisema Maalim Seif analazimika kufanya jambo moja kati ya hayo matano na kuibuka kwa wazee hao wa Chadema jana ni dalili kwamba huenda ameanza kufanyia kazi hoja ya kuihama CUF.

“Sasa hivi CUF ikipasuka Zanzibar, Chadema inachukua nafasi na tunamkaribisha Maalim na wabunge wake waje Chadema kwa sababu sisi ni kitu kimoja,’’ Mwenyekiti wa Baraza Wazee wa Chadema, Hashim Juma aliwaambia waandishi wa habari jana.

Alisema lengo la upinzani ni kuhakikisha maendeleo yanakuwapo nchini hivyo kwa kuwa CUF ipo katika mgogoro Maalim Seif anaweza kuhamia Chadema kwenye nafasi ileile na atapata nafasi ya kuwania urais.

Mbali ya Maalim Seif, Juma alisema anajua CUF ikipasuka Zanzibar, hata wabunge wake watachukua fomu na kuhamia Chadema wote.

Hata hivyo, Maalim Seif alishawahi kukaririwa na gazeti hili akisema hana mpango wa kuhama CUF na jana naibu katibu mkuu wa chama hicho, Nassoro Mazrui alisisitiza kwamba Maalim hawezi kukubali kuwania urais kupitia Chadema hata siku moja.

Alisema ana uhakika mgogoro wao utamalizika na Maalim ataendelea kuwa katibu mkuu na kwamba suala la kuwania urais kupitia chama kingine halipo.

“Maalim hawezi kabisa kuhamia chama kingine kwa sababu ana wafuasi wake huku na wanaujua msimamo wake hivyo kinachotakiwa ni kuomba hatima ya mgogoro wa chama ufikie mwisho tu lakini sio Maalim kuwania urais kupitia huko (Chadema),’’ alisema.

Kuhusu hilo, msemaji wa chama hicho, Mbarala Maharagande alisema hilo la Chadema ni wazo zuri lakini uamuzi mgumu kama huo unatakiwa kutolewa na vikao vya Baraza Kuu la CUF.

“Ni kweli tumepokea ombi hilo, ingawa sijajua wamekaa na Maalim wakaongea kuhusu hili. Muda ukifika baraza litafanya uamuzi’’ alisema na kuongeza kuwa mgogoro wa chama hicho utamalizika Oktoba.

Walichosema wachambuzi

Katika mahojiano na Mwananchi Juni mwaka jana, wachambuzi mbalimbali walitoa maoni tofauti kuhusu hatima ya Maalim Seif.

Katika ushauri wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema mwanasiasa huyo anapaswa kutafuta njia ya kuzungumza na Profesa Lipumba ambaye tayari alikwishaonyesha utayari wa mazungumzo.

Alisema viongozi hao wawili wana nguvu ndani ya chama, hivyo ni jambo la busara wakikutana kuzungumzia tofauti zao na kuendelea kufanya kazi pamoja ili kukijenga chama chao ambacho kina nguvu hasa upande wa Zanzibar.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) alisema kitu anachokiona ni Maalim Seif kwenda kuanzisha chama chake cha siasa ambacho kitatoa ushindani mkubwa kwa CUF.

“Unajua Maalim Seif ana mtaji mkubwa wa wafuasi, kwa hiyo akiamua kuondoka CUF na kuanzisha chama chake atapata nguvu kubwa na chama hicho kitatoa ushindani kwa CCM na CUF yenyewe,” alisema Profesa Mpangala.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), John Samba alisema mpasuko ndani ya CUF ndiyo utakaomfanya Maalim Seif kuachana na siasa kwa sababu anakosa nguvu kutoka kwenye taasisi za umma.

Samba alisema siasa za Tanzania ni ngumu kwa sababu hakuna mazingira sawa na kila chama cha siasa kinaangalia masilahi yake hata kama vitashirikiana. Alisema mgogoro uliopo ndani ya CUF umempunguzia nguvu Maalim Seif katika siasa zake baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.

“Maalim Seif amekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu, nadhani ni wakati aachane na siasa. Sasa hivi naona mambo yamekuwa magumu kwake kwa sababu upande mwingine (wa Lipumba) unapata legitimacy (uhalali) kuliko upande wake,” alisema.

More From Mwananchi
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept