Chadema yasema Wema alikuwa shabiki tu

Muktasari:

  • Hata hivyo, Wema bado hajatoka hadharani kueleza uamuzi wake wa kurudi CCM, ambayo imemuwekea mazingira tofauti na ya watu wengine waliojiunga na chama hicho tawala hivi karibuni.

Siku moja baada mjadala kuhusu kurudi CCM kwa Wema Sepetu, Chadema imesema msanii huyo huyo maarufu wa filamu hajawahi kuwa mwanachama wake bali shabiki wa kawaida.

Hata hivyo, Wema bado hajatoka hadharani kueleza uamuzi wake wa kurudi CCM, ambayo imemuwekea mazingira tofauti na ya watu wengine waliojiunga na chama hicho tawala hivi karibuni.

Si Wema wala mama yake mzazi waliopatikana kuzungumzia suala hilo, ingawa mzazi huyo aliieleza Mwananchi mapema wiki hii jijini Nairobi kuwa hakukuwa na mpango huo.

Lakini juzi usiku, Wema aliandika katika ukurasa wake wa Instagram akisema: “Siwezi kuendelea kuishi kwenye nyumba inayo nikosesha amani. Peace of mind is everything for me. Natangaza rasmi kuondoka Chadema na kurudi nyumbani.”

Wema, ambaye alivuma kutokana na ushiriki wake katika filamu ya My Valentine aliyoigiza na nyota wa sinema Tanzania, Steven Kanumba, alitangaza kuhamia Chadema mapema mwaka huu, akisema CCM ilimuacha pekee katika matatizo yaliyokuwa yanamkabili.

Wakati huo, Wema alikamatwa, kupekuliwa, kupimwa kama anatumia dawa za kulevya na baadaye kufunguliwa mashtaka ya tuhuma za kukutwa na msokoto mmoja wa bangi.

Ilikuwa ni takriban mwaka mmoja baada ya Wema kuendesha kampeni ya “Mama Ongea na Mwanao” iliyolenga kuhamasisha vijana kuipigia kura CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Hata hivyo, Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha) umesema mrembo huyo wa Tanzania mwaka 2006, hakuwahi kuwa mwanachama na hakukabidhiwa jukumu lolote katika operesheni za chama hicho kikuu cha upinzani.

“Wema alikuwa shabiki wa Chadema na Chadema ina wafuasi wa namna mbalimbali,” alisema mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi jana.

“Wapo tunaowafahamu na tusiowafahamu. Wema hakuwa chochote ndani ya Chadema. Wema hakuwahi kufanya ‘movement’ yoyote. Msiwe mnasema amerudi, kwani anatoka wapi?

“Wema hakuwahi kupewa kadi yoyote ya Chadema. Alikuja kwa matatizo yake na ameondoka kwa matatizo yake lakini hakuwa na sifa hata ya kuwa mjumbe wa nyumba kumi.”

Ole Sosopi aliyeteuliwa juzi na Kamati ya Utendaji ya Bavicha kuwa kiongozi wake, alisema kwa sasa Chadema inapitia kipindi muhimu kitakachoiimarisha.

“Tuna taarifa za watu wengine kuondoka, wacha waondoke. Jiulize mwenyekiti wa Bavicha (Patros) Katambi ameondoka peke yake. Ameshindwa kumchukua hata mwenyekiti wa Bavicha wa Kata. Wema ameondoka peke yake, wacha waondoke,” alisema Ole Sosopi.

Lakini katibu wa itikadi wa CCM, Humphrey Polepole alionekana kumuwekea mazingira tofauti.

“Tumeweka katika katiba kuwa wanaporudi wanaohama, hatuwakubali mpaka tufanye uchunguzi wa kutosha kama dhamira yao ni njema. Chama chetu si kama daladala ambalo unapanda, unashuka ili mradi una nauli.”

Lakini watu wengine watano waliojiunga na CCM hivi karibuni, walipewa nafasi ya kuzungumza mbele ya Halmashauri Kuu iliyofanya kikao chake Ikulu.