Chadema yasema haitambui matokeo Siha, Kinondoni

Muktasari:

Wagombea wa CCM katika majimbo ya Siha na Kinondoni ndiyo wameibuka washindi.


Dar es Salaam. Chadema imesema haitambui matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika katika majimbo ya Siha na Kinondoni jana Februari 17,2018.

Chama hicho katika taarifa iliyotolewa jana usiku hata kabla ya matokeo kutangazwa, kimesema yamepatikana kinyume cha Katiba ya nchi, sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi.

Taarifa hiyo iliyotolewa na katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji iliwaagiza mawakala wa chama hicho wasiende kwenye vituo vya majumuisho ya kura katika majimbo hayo.

Matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Siha yalitangazwa jana usiku ambayo Dk Godwin Mollel wa CCM ameshinda kwa kupata kura 25,911; Elvis Mosi wa Chadema (5,905); huku Tumsifuel Mwanri wa CUF akipata kura (274) na Azaria Mdoe wa SAU (170)

Watu walioandikishwa kupiga kura walikuwa 55,313, waliojitokeza walikuwa 32,277 na kura halali zilikuwa 31,960.

Wakati huohuo, msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya  Kinondoni, Aron Kagurumjuli ametangaza matokeo ya Kinondoni leo Februari 18,2018.

Amesema Maulid Mtulia wa CCM ameshinda kwa kupata kura 30,247 akifuatiwa na Salum Mwalimu wa Chadema aliyepata kura 12,353 na Rajab Salum wa CUF aliyepata kura 1,943.

Dk Mashinji katika taarifa hiyo amedai uchaguzi uligubikwa na vitendo viovu dhidi ya demokrasia na uchaguzi wenyewe.

Amedai katika jimbo la Kinondoni, Tume imefanya urasimu kinyume cha sheria na makosa ya makusudi ikiwamo kutolewa mawakala wao kwenye vituo vya uchaguzi.

Kuhusu jimbo la Siha, amedai vyombo vya dola na hasa Jeshi la Polisi lilitumika vibaya kwa kuwalazimisha mawakala kusaini fomu za matokeo tofauti na fomu rasmi zilizoko vituoni.

Pia, Chadema imewatuhumu polisi kwamba wametumika kupora masanduku na kubandika matokeo vituoni bila kujulikana yametoka wapi.

Amedai kumekuwa na vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wagombea, viongozi wa Chadema na raia wengine wasio na hatia katika maeneo kulikofanyika uchaguzi mdogo,  huku vyombo vya dola na NEC wakikaa kimya.