Chadema yataka wanaojiengua watoe sababu halisi

Muktasari:

  • Chadema imesema iko imara na haiyumbishwi na wimbi la watu wachache ambao wameamua kuwasaliti wapiga kura.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wanachama wake wanaoondoka na kujiunga na CCM kueleza sababu halisi zinazowafanya kuhama na si kuwahadaa Watanzania.

Chadema imetoa kauli hiyo muda mfupi baada ya aliyekuwa mbunge wake wa Siha, Dk Godwin Mollel kutangaza kujivua uanachama na ubunge kwa kile alichoeleza anakwenda kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais John Magufuli.

Taarifa ya Chadema iliyotolewa leo Alhamisi Desemba 14,2017 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema imesema kuondoka kwao hakuwezi kukiyumbisha chama hicho.

Amesema sababu alizozitoa Dk Mollel ni za kushangaza kwa kuwa Bunge ndilo lenye wajibu wa kusimamia na kulinda rasilimali za Taifa kwa niaba ya wananchi.

“Sasa huyu anakimbia bungeni anakuja uraiani sijui atatumia miujiza gani maana kalikimbia Bunge lenye wajibu huo kwa mujibu wa Katiba na sheria zetu. Tunawashauri wale wote ambao wanajitoa waeleze sababu halisi na si kuhadaa umma kwa sababu uchwara kama hizi,” amesema Mrema.

Amesema, “Maana wapo wanaosema wanaacha kazi kwenda kuunga mkono dhana ya hapa kazi tu na wengine wanasema wanaenda kuunga mkono juhudi za kuboresha maisha kwa kuacha kazi.”

Mrema amesema Chadema iko imara na itaendelea na ajenda zake bila kuyumbishwa na wimbi la watu wachache ambao wameamua kuwasaliti wapiga kura kwa sababu ambazo hazina masilahi kwa Taifa bali wao binafsi.

“Tutaendelea kujenga Taifa na chama chetu bila kujali njaa za baadhi yetu ila kwa hakika ni kuwa, wale wenye dhamira thabiti ndio wataweza kufika mwisho wa safari salama, ila kwa hakika wenye njaa ya akili na tumbo safari hii hawataweza kufika mwisho wake,” amesema Mrema.