Chadema yazungumzia kuzama kwa Kivuko, yamtaka Rais Magufuli...

Muktasari:

Mbunge pekee aliyetoa tahadhari ya kutokea kwa maafa kwenye kisiwa hicho ni wa Ukerewe (Chadema) Joseph Mkundi, jambo ambalo lilipata majibu badala ya majawabu kutoka Serikalini.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema ajali iliyotolewa Ukerewe jijini Mwanza ya kuzama Kivuko cha Mv Nyerere ni ya kizembe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 21, 2018 kuhusu ajali iliyotokea Ukerewe jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wanamtaka Rais John Magufuli achukue hatua kwa watendaji wake.

Amesema safari kutoka Kisiwa vya Bugorora hadi Ukara ni ya dakika 45 na kina uwezo wa kubeba abiria 101 lakini inasemekana ilibeba zaidi ya abiria 400 na mizigo.

Mbowe amesema Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Joseph Makundi amekuwa akilalamika sana suala la kuwapo kwa kivuko hicho kimoja  lakini hakupata muafaka.

Amesema kumekuwa na marudio ya matukio ya ajali za namna hiyo na Taifa hadi sasa halina mbinu za kujikinga wala kuokoa.

Amesema boti jana ilizama mapema saa 8 mchana na hadi inafika saa 12:00 jioni hakuna utaratibu uliofanyika wa kuandaa vifaa vya uokoaji.

Amesema ajali imetokea mita 100 kutoka ufukweni lakini inashindikana  kufanya uokoaji.

"Kwa jana tulilidhika waliokuwa ndani ya maji wote wamekufa, kwa sababu mtu hawezi kulala kwenye maji halafu useme utamuokoa kesho,” amesema Mbowe

"Hatuna vifaa vya kisasa vya uokoaji kwenye maziwa makubwa Nyasa, Viktoria, waliokuwa wanajaribu kuokoa ni wavuvi ambao hawana oksijeni wala vifaa vya kisasa vya uokoaji," ameongeza

 

Mbowe amefafanua kuwa hiyo inatokana na kutokuwa na tabia ya kuwajibika.

Amesema kuna watu wa Temesa, Sumatra, Navy na Polisi wa majini na hakuna anayetoa maelezo ya kina wala kuwajibika.

Ameeleza wanawaomba Watanzania waungane wapige kelele awajibike mtu katika uzembe huo.

"Mawaziri utawasikia wanasema mimi sikuhusika, kama wangefanya kwa weledi hili lisingetokea, tunapoteza maisha ya watu kwa uzembe uliotukuka," amesema Mbowe.

Amesema Chadema inamtaka Rais achukue hatua awawajibishe  watendaji wake kwa uzembe huo.

Amefafanua asiseme hachukui hatua kwa sababu Mbowe amesema.

"Nimesema  kama Mtanzania" amesema.

Ameeleza vivuko havitoshi, kuna taarifa Serikali ina mpango wa kuongeza kivuko sawa, ila bado havitoshi.

 

Amesema  visiwa vinahitaji boti kwa sababu cha Mv Nyerere kilizinduliwa na Rais wa awamu ya  tatu  Benjamini Mkapa miaka zaidi ya 10  iliyopita.

"Ninawaambia Serikali haitatoa idadi ya watu waliokufa kwa sababu hakuna utaratibu wa kuwatambua watu kwa idadi na majina.

"Kuna taarifa kuwa kuna gari za mizigo zimesizama na mahindi zaidi ya gunia 100 zimezama," amesema Mbowe.

Amesema wanamtaka Rais Magufuli  azungumze na Taifa na awape pole wananchi, atoe siku za maombolezo haitoshi kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa kutoa taarifa.

Amesisitiza wanaitaka Serikali ijiandae kulipa fidia kwa familia zilizopita watu na mali.

"Kuna taarifa kuwa kulikuwa na maboya mchache watu walikuwa wananyang'anyana na  yaliyokuwapo yalikuwa kwenye chumba kilichofungwa," amesema Mbowe.

Mbowe amesema wao kama chama wanasubiri kwa unyenyekevu mkubwa kuungana na taifa kuomboleza kadri wenye dhamana watakavyotoa maelekezo.