Chakula kipo lakini bei imepanda -RC

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo.

Muktasari:

Akizungumza jana baada ya kutembelea masoko, Ndikilo alisema licha ya ziada hiyo, pia alikuta vyakula aina mbalimbali sokoni vikisubiri wanunuzi lakini amebaini bei imepanda na hasa unga wa sembe na viazi mbatata kutokana na soko kuwa huria.

Kibaha. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema mkoani hapa kuna ziada ya tani 503,711.5 za chakula.

Akizungumza jana baada ya kutembelea masoko, Ndikilo alisema licha ya ziada hiyo, pia alikuta vyakula aina mbalimbali sokoni vikisubiri wanunuzi lakini amebaini bei imepanda na hasa unga wa sembe na viazi mbatata kutokana na soko kuwa huria.

“Chakula kipo cha kutosha lakini nimeshuhudia bei imepanda na hasa viazi mbatata na sembe ambayo kilo moja inauzwa hadi Sh1,500 kwa kilo,” alisema.

Alisema katika msimu wa kilimo uliopita (2015/16) licha ya hali ya mvua za vuli na masika kuwa mbaya, mkoa ulivuna tani 773,279 za chakula cha wanga na mikunde tani 10,144, huku mahitaji yakiwa ni tani 269,568 kwa watu 1,136,218 wa mkoa huo kwa mujihu wa Sensa ya Watu na Makazi.

Ndikilo alisema takwimu hizo zinaonyesha mkoa una ziada ya tani 503,711 za chakula kwa wakulima, ambao aliwashauri kukitumia vizuri na kuweka akiba kwa kuwa hali ya hewa haitabiriki.

“Nashauri endeleeni shughuli halali, endapo kutatokea hali mbaya ya uhaba wa chakula na Serikali ikajiridhisha basi wananchi hawawezi kuachwa wafe njaa, Serikali ina akiba ya kutosha,” alisema.

Ndikilo aliwaagiza wakuu wa wilaya na wataalamu wa kilimo kuwahimiza wananchi kutunza akiba ya chakula waliyonayo, walime mazao yanayokomaa kwa muda mfupi, mahindi maeneo ya mabondeni na mazao yanayostahimili ukame.

Mwenyekiti wa Soko B lililopo Chalinze, Jafari Waziri alisema vyakula vipo lakini kinachowasumbua wananchi ni ugumu wa upatikanaji wa fedha kutokana na mzunguko kuwa mdogo.

Alisema wananchi wengi hutegemea biashara ndogondogo ikiwamo ya ufuta ambao ulinyauka msimu uliopita na pia, vitu vimepanda bei kutokana na usafirishaji kwa kuwa hununua Ifakara mkoani Morogoro na Mbeya.

Mkazi wa Mlandizi, Vivian Pater alisema Serikali iwaamuru wafanyabiashara kuiingiza sokoni chakula ili kuondoa kero ya kupanda bei ya bidhaa hizo na hasa sembe ambayo kila muuzaji anadai imepanda kwa kuwa mahindi hayapatikani.