Chanzo cha ukosefu wa dawa zahanati chatajwa

Muktasari:

  • Uanzishwaji wa wakala wa ununuzi wa dawa utakuwa na maana endapo mikataba itakayoandaliwa itafuatwa na kusimamiwa

 Serikali imetaja sababu za kukosekana kwa dawa katika zahanati na vituo vya afya maeneo mbalimbali nchini kuwa kunatokana na ukiritimba wa taratibu za ununuzi na mabadiliko ya bei mara kwa mara.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Josephat Kandege alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akifungua kongamano la pamoja kwa wadau wa afya lililoandaliwa na Serikali kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la HPSS.

Lengo la kongamano hilo ni kuangalia mfumo mzuri wa kuwa na mzabuni mmoja au wawili kwa kila mkoa atakayepewa kazi ya kununua dawa.

Kandege alisema Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuhakikisha dawa zinakuwapo katika vituo wakati wote.

“Mbali na hayo, lakini baadhi ya watumishi wetu wamekuwa si waaminifu kabisa, hivyo kusababisha matatizo makubwa kwa kushirikiana na wazabuni ambao nao hawana uzalendo kwa nchi yetu,” alisema Kandege.

Alifafanua kuwa Serikali kwa upande wake imekuwa ikitimiza wajibu wake ikiwamo kutenga fedha za kutosha katika bajeti yake.

Kandege alisema mwaka 2015/16 zilitengwa Sh31 bilioni lakini 2017/18 zilitengwa Sh 236 bilioni jambo linaloonyesha ukuaji wa bajeti katika eneo hilo.

Mratibu wa menejimenti ya dawa wa Shirika la HPSS, Fiona Chilunda alisema shirika lilianzisha mradi huo baada ya kubaini matatizo ya upatikanaji wa dawa kuwa chini ya asilimia 60 licha ya fedha katika maeneo husika kuwapo.

Chilunda alisema katika uchunguzi wao walikuwa wamebaini uwapo wa fedha nyingi serikalini lakini utaratibu mbovu wa ununuzi wa dawa ndiyo ulikuwa ukiwapa adhabu ya kukosa dawa.

Kuhusu uanzishwaji wa wakala wa ununuzi wa dawa alisema utakuwa na maana endapo mikataba itakayoanadaliwa itafuatwa na kusimamiwa vema.

Mkurugenzi wa Afya, Ofisi ya Rais Tamisemi, Ntuli Kaporogwe alisema mfumo huo unaojulikana kama ‘vendor system’ utakuwa imara na mzuri wenye kuondoa kero za kutokuwepo kwa dawa.

Kaporogwe alisema kwamba majaribio ya mfumo huo waliyafanya na HPSS na kuonyesha mafanikio kwa mikoa ya Dodoma, Morogoro na Shinyanga lakini kwa sasa wanataka kufanya mpango huo uwe wa nchi nzima.