China, Afrika wakubaliana mambo matatu

Muktasari:

Pia, vimekubaliana kuwa na mikakati ya kuwaletea wananchi maendeleo badala ya kujikita zaidi katika kupata kura wakati wa uchaguzi.

Dar es Salaam. Vyama vya siasa 40 kutoka nchi za Afrika na Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), vimeridhia mambo matatu ikiwamo kuimarisha umoja, mageuzi ya kiuchumi na kuchagua njia sahihi za kuondoa umaskini
Pia, vimekubaliana kuwa na mikakati ya kuwaletea wananchi maendeleo badala ya kujikita zaidi katika kupata kura wakati wa uchaguzi.
Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema hayo akiwasilisha maazimio ya mkutano uliovishirikisha vyama hivyo jijini Dar es Salaam.
Vyama hivyo vilitumia mkutano huo kubadilishana uzoefu kwa kila kimoja kuwasilisha taarifa, huku China ikieleza namna ilivyofanikiwa kiuchumi na dhamira yake ya kuisaidia Afrika.
“Tumemaliza ngwe ya kwanza ya kupambana na ukoloni, kupokwa rasilimali zetu, kudhalilishwa kwa misaada yenye masharti magumu sasa tunaenda kuijenga Afrika iliyo imara kiuchumi, tumekubaliana,” alisema Dk Bashiru.
Alisema vyama hivyo vimeridhia kujifunza kutoka China namna ilivyofanya mageuzi ya kiuchumi na kuimarisha nidhamu kwa viongozi wake.
“Tumekubaliana tukitoka hapa tunaenda kuimarisha vyama vyetu, kila chama kimegundua kuwa siri ya kutuondoa tulipo ni kujifunza kwa CPC namna ilivyopambana na rushwa, ufisadi, ubadhilifu wa mali na kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Dk Bashiru.
Katibu mtendaji wa Baraza la Vyama vya Siasa Afrika, Najie Ahmed alisema sababu za matatizo mengi katika mataifa hayo ni kuwapo kwa migogoro ya wenyewe kwa wenyewe na utegemezi wa misaada yenye ajenda za kisiasa.
Alisema ili nchi iendelee inahitaji kufanya mageuzi makubwa kiuchumi bila kuchezea tunu za Taifa zilizopo.
Najie alisema kila upande umekubali kujifunza kwa mwingine ili baadaye kuwe na mfumo wa namna ya kufikia uchumi wa kati.
“Uhusiano huu tunaoimarisha unalenga kuongeza uzalishaji wenye tija, ni lazima tusimame imara ili kukabiliana na changamoto zinazotuzunguka,” alisema.
“Tunataka uhusiano wetu ulenge kujenga na kuwekeza kwenye viwanda ili nchi zetu ziimarishe na kukuza sekta ya kilimo. Miaka kadhaa ijayo tunataka kuiona Afrika iliyo na uchumi imara.”
Akifunga mkutano huo ulioanza juzi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliwataka viongozi hao wanapokwenda kutekeleza makubaliano hayo wasisahau jitihada za waasisi wa vyama hivyo.
“Nchi za Afrika zinahitaji kuwa huru kiuchumi, safari hii haitaweza kukamilika kama mtasahau jitihada za waasisi wa vyama vyenu. Pia, viongozi wataendelea kuongoza kwa ubabe, kujilimbikizia mali, rushwa na ufisadi,” alisema.
Alisema nchi za Afrika zina kila sababu ya kujifunza kutoka China namna ilivyoweza kuwakomboa wananchi kutoka katika umaskini. “Kama isingekuwa China, umaskini duniani ungeendelea kuwa juu. Kama ingekuwa ni kutoa tuzo kwa nchi iliyopiga hatua kiuchumi basi China inastahili kupata,” alisema.
Balozi Iddi alisema Tanzania imenufaika na ujenzi wa miradi mingi kwa msaada wa China ukiwamo wa Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara).
“Nchi hustawi kwa vitendo na si kwa maneno, utekelezaji wa maazimio yenu ukafanyike kwa vitendo, vinginevyo mkutano huu wa kihistoria hautakuwa na maana kwetu,” alisema.
Naibu waziri wa Mambo ya Nje wa CPC, Xu Lyping alisema ni wakati wa vyama vya siasa kuaminiana na kuweka misingi imara ili vifikie ndoto ya kiuchumi waliyokubaliana.
Alisema China iko tayari kufanya kazi na Afrika, na uhusiano ulioanzishwa miaka mingi iliyopita hawataukatisha.
“Kesho ipo mikononi mwa wanaojiandaa leo, maandalizi yetu mazuri ndiyo mafanikio yetu kiuchumi baadaye. China tulifanya hivi na sasa ni Taifa kubwa linalojitegemea kiuchumi,” alisema.
Alisema wanaandaa mkutano mwingine kama huo Beijing ambao vyama vya siasa vya Afrika kila kimoja kitakuwa na mkakati wenye kipaumbele katika kuutekeleza.
Naibu waziri huyo alisema China iko tayari kuendelea kufanya kazi na Afrika katika kupambana na umaskini.

Afrika yaumwa sikio
Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wakizungumzia mkutano huo, walisema kama nchi za Afrika zitaitumia fursa hiyo ipasavyo zitaweza kujikwamua kiuchumi.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Isdory Sothenes alisema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo, hivyo imepata uzoefu wa kutosha wa namna ya kuwasaidia wananchi na kukuza maendeleo.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema mkutano huo ni fursa adhimu kwa Afrika katika uchumi iwapo itatekeleza makubaliano yaliyofikiwa.
“Kila upande umejifunza kutoka kwa upande mwingine na wametoka na makubaliano ya pamoja, kama watakwenda kuyafanyia kazi basi miaka ijayo Afrika itakuwa si hii ya sasa,” alisema Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi.
Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda alisema kinachoitofautisha China na Afrika ni tamaduni.
“China wana utamaduni wa aina moja lakini Afrika tunatofautiana. Tuna makabila mengine na tamaduni nyingi, hivyo hatutaweza kuiga kila kitu lakini kila nchi inaweza kuwekeza kulingana na mazingira yake,” alisema.
Mchambuzi wa uchumi, Moses Mwizarubi alisema makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa katika mkutano huo ni msingi imara wa uchumi wa Afrika.
“Mahusiano haya yanapaswa kuwa na kipaumbele. Uwekezaji unaozungumzwa unapaswa kuelekezwa kwenye miundombinu, kilimo, nishati, viwanda na ushirikiano kibiashara,” alisema.