China kuifanyia marekebisho Reli ya Tazara

Muktasari:

Balozi Msaidizi wa China nchini, Guo Haodong amesema mpango huo ni katika kuimarisha undugu kati ya nchi hizo ambao ulianza miaka mingi iliyopita.

Dar es Salaam. Serikali ya China imesema  ina mpango kufanyia maboresho  Reli ya Tazara na kwa sasa mpango huo upo katika hatua ya mazungumzo ya ujenzi huo unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao.

Balozi Msaidizi wa China nchini, Guo Haodong amesema mpango huo ni katika kuimarisha undugu kati ya nchi hizo ambao ulianza miaka mingi iliyopita.

Akizungumza katika maonyesho ya picha za reli ya Tazara zilizochorwa na wasanii kutoka China, Haodong amesema michoro hiyo ni kumbukumbu  kwa vizazi vijavyo kwa sababu hakukua na taarifa zozote katika nyumba za sanaa na maonyesho kuhusu reli hiyo.

"Tazara ilijengwa na Jamhuri ya watu wa China miaka mingi iliyopita kwa kushirikiana na wazawa lakini si Tanzania wala China ambazo zimehifadhi  kumbukumbu hii  licha ya umuhimu mkubwa kwa nchi wanachama," amesema balozi huyo.