VIDEO: Chiza wa CCM ashinda Buyungu

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Buyungu wilayani Kakonko mkoani Kigoma, Lusubilo Mwakabibi, akimkabidhi cheti cha ushindi Christopher Chiza mara baada ya kutangazwa matokeo mapema leo saa 11 alfajiri. Picha na Happiness Tesha.

Muktasari:

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili Agosti 12, 2018, Chiza amepata kura 24,578 akifuatiwa na Eliya aliyepata kura 16,910.


Kakonko. Christopher Chiza (CCM) ameibuka mshindi katika uchaguzi wa ubunge jimbo la Buyungu mkoani Kigoma baada ya kuwashinda wapinzani wake wanane, akiwemo mgombea wa Chadema,  Eliya Michael.

Katika uchaguzi huo uliofanyika jana Jumapili Agosti 12, 2018, Chiza amepata kura 24,578 akifuatiwa na Eliya aliyepata kura 16,910.

Akitangaza matokeo hayo leo Jumatatu Agosti 13 saa 11 alfajiri, msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Lusubilo Mwakabibi amemtangaza Chiza kuwa mshindi.

Vyama vingine na kura walizopata ni Demokrasia Makini (11), UMD (12),  NRA (17), UPDP (18), DP (22), AFP (51) na  ACT – Wazalendo kura 100.

Mwakabibi amesema idadi ya waliojiandikisha kupigakura ni  61,980, waliopiga kura ni 42,356, kwamba  kura halali zilikuwa 41,841 na zilizoharibika 515.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Chiza amesema yupo tayari kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo na kuwaahidi utumishi uliotukuka.

Amesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi na akiapishwa ataanza nazo mara moja.

Awali, Eliya amesema mawakala wake hawakuitwa kwenda kujumlisha matokeo hayo, kubainisha kuwa uchaguzi huo ulikuwa na mazingira magumu.

Amesema matokeo aliyonayo kutoka katika kila kituo, hayafanani na yaliyotangazwa.

“Kwa umri nilionao najiona mshindi wa uchaguzi huu, nimejifunza mengi na umenijenga kwa kiwango kikubwa. Nimeshinda kwa kura za watu ili wao wameamua kumtangaza mtu wanayemtaka,” amesema.