Ali Choki aitosa tena Twanga Pepeta

Muktasari:

Alirejea Twanga Pepeta mwaka 2015 baada ya kuvunjika kwa bendi yake ya Extra Bongo.

 

Dar es Salaam. Mkataba wa mwanamuziki Ali Choki na bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta unamalizika Machi, 2018 na inaelezwa kuwa hataongeza mkataba mwingine.

Akizungumza leo Februari 5, 2018 mmiliki wa Twanga Pepeta, Asha Baraka amethibitisha Choki kuondoka baada ya kumrudisha katika bendi hiyo mwaka 2015 akitokea bendi ya Extra Bongo.

Amesema Choki ni kama mwanae amempa nafasi ya kutafuta riziki sehemu nyingine na iwapo atakwama atamkaribisha tena Twanga Pepeta.

Kwa upande wake, Choki  aliyetunga nyimbo mbalimbali kama Aminata na Chuki Binafsi amesema anaanzisha bendi nyingine na kwamba kinachomuondoa Twanga Pepeta ni maslahi.

“Naona bora kwenda kufanya kazi mwenyewe. Katika bendi hiyo sitarajiii kuajiri  mwanamuziki yoyote. Nikiwa na onyesho nitawachukua wanamuziki mbalimbali na tukimaliza nawalipa, kila mmoja kuendelea na shughuli zake,” amesema.

Amesema tayari ameanza kuandaa nyimbo kwa ajili ya bendi yake hiyo, na mwaka huu atatoa nyimbo saba.

Alipoulizwa kama atakuwa tayari kushiriki upigaji video wa nyimbo alizoimba akiwa Twanga Pepeta amesema, “Nitakuwa tayari kupiga picha za video kama watanihitaji kwa sababu sina ugomvi nao.”

Amesema atakuwa mwanamuziki huru, hivyo Twanga Pepeta wanaweza kumuita katika maonesho yao na kumlipa.

Amebainisha kuwa kitendo cha Twanga Pepeta kutofanya video kama miaka ya nyuma ni moja ya sababu inayomuondoa katika  bendi hiyo.

“Hiki ndio kinachofanya muziki wa dansi ushuke nchini, tumeshindwa kuutendea haki kwani hatuutangazi hata katika mitandao ya kijamii. Tumebaki kusubiri nyimbo zetu zichezwe kwenye televisheni huku tukijua dunia imebadilika. Hapa hakuna wa kumlaumu  tujirekebishe,” amesema.