Chuo Kikuu Huria kutoa shahada ya ualimu Veta

Dar es Salaam. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), kitaanza kutoa shahada ya ualimu ya ufundi kwa wanafunzi waliosoma masomo yanayohusu utoaji wa huduma za ufundi (Veta).

Hayo yalisemwa jana na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Elifasi Bisanda alipokuwa akisaini mkataba na Chuo cha Ufundi Veta utakaowezesha OUT kuwapokea wanafunzi baada ya kuhitimu mafunzo mbalimbali ya ufundi.

Profesa Bisanda ambaye ni mratibu wa mpango huo alisema atahakikisha anafanikisha kwa kiwango cha juu ili kueandana na teknolojia ya wakati huu.

Alisema kutokana na sera ya viwanda ni muhimu kutoa elimu ya mafunzo ili kila atakayemaliza Veta awe na vigezo na sifa za kufundisha wengine ili kuzalisha wataalamu zaidi.

Aliongeza kuwa baada ya kibali kupatikana mpango huo utaanzia makao makuu Morogoro, baadaye utaendelea kwenye mikoa mingine ili kuwafikia Watanzania wote watakaohitimu mafunzo ya ufundi.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Veta Morogoro, Anamringi Maro alisema Veta wamekuwa wakiajiri watu ambao hawajapata mafunzo ya ualimu na kuwa na taaluma katika ufundishaji, hivyo mpango huu utasaidia kupata wataalamu wa kutosha katika vyuo vya ufundi.

Aliongeza kuwa kutokuwa na walimu wenye sifa kunachangia kutofuata mitaala, hivyo mpango huu utakapoanza utasaidia kufundisha kwa kufuata mitaala ya Veta.