Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilivyojiimarisha kuwa kitovu cha Kiswahili duniani

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala

Muktasari:

UDSM inayoongozwa na Profesa Rwekaza Mkandala, ambaye ni makamu mkuu wa chuo, imefanikisha lugha ya Kiswahili kupiga hatua nchini na ulimwenguni kutokana na kuzalisha wataalamu ambao wamekuwa chachu ya kukieneza katika mataifa mbalimbali kama Zimbabwe, Afrika Kusini, Rwanda, Ujerumani na Marekani.

Kwa kiasi kikubwa chimbuko la mabadiliko yanayohusu lugha ya Kiswahili Afrika Mashariki, barani Afrika na dunia nzima, ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

UDSM inayoongozwa na Profesa Rwekaza Mkandala, ambaye ni makamu mkuu wa chuo, imefanikisha lugha ya Kiswahili kupiga hatua nchini na ulimwenguni kutokana na kuzalisha wataalamu ambao wamekuwa chachu ya kukieneza katika mataifa mbalimbali kama Zimbabwe, Afrika Kusini, Rwanda, Ujerumani na Marekani.

UDSM, kwa kutumia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki), imekuwa chachu ya mabadiliko kutokana na kusaidia lugha hiyo kukua na kutanuka. Chuo hicho kikongwe nchini kimeimarisha ushirikiano na mataifa hayo kwa kutumia wanazuoni wake ambao wamekuwa katika mapambano kuhakikisha Kiswahili kinafundishwa vyuo vikuu.

Tafiti za kisayansi na machapisho mbalimbali, ambayo yametolewa tangu Tataki ikijulikana kama Idara ya Kiswahili na baadaye kuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), ni miongoni mwa mambo ambayo yamekifanya chuo hicho kuendelea kuwa kitovu cha lugha ya Kiswahili duniani.

Kwa wanafunzi wengi wanaotoka nje ya nchi, chuo hicho kimekuwa kimbilio lao la kujifunzia lugha ya Kiswahili.

Katika utawala wa Profesa Mukandala tumeshuhudia mabadiliko mengi katika taasisi ya Kiswahili kwa kuamua kukitumia kuwa lugha rasmi ya mawasiliano chuoni hapo, kama katika vikao vya utawala na vinavyohusu wanafunzi na menejimenti.

Kutokana na mafanikio hayo, bila shaka vyuo vingine vinaweza kuamua kuiga jambo hilo lenye masilahi kwa Taifa. Hiyo ni hatua kubwa katika maendeleo ya Kiswahili nchini na duniani.

Kiswahili katika baadhi ya kozi

Uamuzi wa chuo hicho kuanza kufundisha baadhi ya kozi kwa Kiswahili ni jambo linaloifanya UDSM kuwa ya kwanza nchini kuendeleza lugha hiyo. Bila ya shaka, utekelezaji wa jambo hilo utakapoanza, utakiwezesha Kiswahili kuthibitika kwamba UDSM ndipo chimbuko lake.

Uamuzi huo umeamsha hisia kwamba lugha ya Kiswahili, ambayo imekuwa ikipigwa teke kwa miaka mingi, sasa inawezekana ikaanza kutumika katika nyanja kama vile uchumi, elimu, sheria, sayansi, teknolojia na maeneo mengine ya mawasiliano

Utafiti uliofanywa na wanataaluma kutoka maeneo mbalimbali duniani unaonyesha kwamba mwanafunzi akifundishwa kwa lugha yake ya kwanza, hupenda kujifunza zaidi na huelewa vyema. Kilichobaki ni Watanzania kuamua wenyewe.

Profesa Mukandala na Kiswahili

Profesa Mukandala ni miongoni mwa viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mawanda ya matumizi ya Kiswahili yanaongezeka.

Kiongozi huyo amekuwa na kiu kuona kwamba lugha ya Kiswahili inaheshimika ndani ya mipaka ya nchi na nje.

Tataki

Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) inayoongozwa na Dk Ernesta Mosha, ambaye ni mkurugenzi, imefanya mambo mengi ikiwamo kufanikisha machapisho ya vitabu vya masomo yote kwa lugha ya Kiswahili, hususan ya elimu ya sekondari.

Taasisi hiyo imekuwa na mchango mkubwa kutokana na kuwaunganisha wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili nchini.

Hivi karibuni iliandaa Tuzo za Mabati Cornel ambazo zililenga kuhamasisha wananchi kuwa na mwamko wa uandishi wa fasihi.

Tanzania ilitoa washindi watatu waliowasilisha muswada wa kazi zao ambazo zilipigiwa kura na jopo la wachambuzi. Mshindi wa kwanza aliibuka na kitita cha Sh10 milioni.

Ushirikiano wa taasisi hiyo na taasisi nyingine uwewezesha kuwaunganisha wazungumzaji wa Kiswahili nchini na kujisikia wakithaminiwa na kuonekana wa thamani kutokana na kuzungumza lugha hiyo.

Mdahalo wa kitaifa wa Kiswahili

Kwa kuona umuhimu wa kuwa na mdahalo wa Kiswahii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliamua kushirikiana na wadau wengine wa lugha hiyo ili kuwawezesha wananchi kufahamu zaidi mwelekeo wa Kiswahili.

Mada iliyoandaliwa kwa ajili ya kujadiliwa katika mdahalo huo, itawapa nafasi wananchi kutoa maoni iwapo Kiswahili kinafaa kwa matumizi katika nyanja zote au la.

Mdahalo huo unatarajiwa kuwa na pande mbili, wanaopinga na wanaokubali kutumia Kiswahili katika nyanja tofauti.

Mdahalo huo utakaorushwa mubashara na vyombo vya habari, utatoa fursa kwa Watanzania kujadili kwa uwazi.

Matokeo ya mdahalo huo

Mdahalo huo utawawezesha watunga sera kuamua iwapo waendelee kutumia lugha za kigeni katika nyanya mbalimbali kama sheria, uchumi, teknolojia na elimu kwa kuwa jambo hilo likipitishwa kwa kauli moja na wananchi walio wengi huenda watunga sera wakalifanyia kazi na kulitungia sheria.

Washiriki wa mdahalo

Mdahalo huo ulioandaliwa na UDSM kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Kiswahili - Kanda ya Tanzania, umelenga kuwashirikisha wananchi wa kawaida, wasomi, wataalamu wengine. Pia utashirikisha wageni kutoka mataifa ambayo tayari yamepiga hatua kwa kutumia lugha zao.

Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki

Kuundwa kwa Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki ambako kuliridhiwa na nchi wananchama, kumekuwa chachu ya kuanzishwa vyama mbalimbali katika kila nchi wanachama.

Chama cha Waandishi wa Habari za Kiswahili - Kanda ya Tanzania kimekuwa chachu katika kutekeleza majukumu yake, kama kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Chama hicho kinachoundwa na waandishi wa habari na watayarishaji wa vipindi vya Kiswahili, kimeibua hamasa mpya nchini pamoja na kuwa sehemu ya waandaaji wa mdahalo huo.

Kamisheni hiyo yenye makao yake makuu visiwani Zanzibar, imefanikiwa kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika nchi wanachama na kuweka hamasa kwa mataifa mengine kama Rwanda, katika kuongeza kasi ya kujifunza lugha ya Kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mchambuzi ni mwandishi wa gazeti hili. Anapatikana kwa simu 0712127912