Serikali yaahidi kuendelea kukijengea uwezo chuo cha Kodi

Muktasari:

Serikali kukiendeleza chuo cha Kodi ili kiweze kuendelea  kuzalisha wataalamu  bora wenye kukidhi  mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Dar es Salaam. Serikali  kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imesema itaendelea kukijengea uwezo Chuo cha Usimamizi wa Kodi Nchini (ITA) ili kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinazalisha wataalamu  bora wenye kukidhi  mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo  Novemba 18 Jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dk Yamungu  Kayandabila wakati wa mahafali ya kumi cha Chuo cha Kodi Nchini (ITA) na kuongeza kuwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinazalisha wataalamu wenye umahiri katika masuala ya forodha na kodi.

Dk  Kayandabila amesema  Serikali inatambua umuhimu wa Chuo hicho kwa ustawi wa kiuchumi na kijamii, hivyo kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itaendelea kukipangia Chuo hicho bajeti ya maendeleo ili kukidhi matumizi yake ya kimaendeleo ikiwemo kufanya tafiti kwa kiwango kinachohitajika.
"Serikali itaendelea kushirikiana na Chuo cha Kodi kupitia Mamlaka ya Mapato kwa kuhakikisha kuwa mipango yenu hususani Mpango Mkakati wa nne unaoanza kutekelezwa mwaka 2017/18 unatekelezwa kikamilifu kwa kuwapatia hosteli mpya za wanafunzi, upanuzi wa majengo ya ofisi za wakufunzi na ujenzi wa kampasi mpya ya Misugusugu Kibaha Mkoani Pwani" amesema.

Dk Yamungu amewataka wahitimu hao kutambua kuwa Serikali inatambua umuhimu na mahitaji ya Wataalamu wa kodi, hivyo Chuo hicho hakina budi kuzalisha wataalamu watakaosaidia juhudi za Serikali za kukuza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi kwa wafadhili.
Ameongeza kuwa pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na Chuo hicho, Dk Kayandabuila ameutaka uongozi wa chuo hicho kuendelea kujiimarisha katika utafiti na kutoa mafunzo katika masuala ya kodi hususani sekta ya uchimbaji madini, mafuta na gesi na sekta ya fedha ili kusaidia kuongeza makusanyo ya mapato katika sekta hizo.

Akifafanua zaidi Kayandabila amesema  utafiti katika sekta za madini, mafuta na gesi utasaidia kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukuza mapato ya ndani na kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma za kijamii na kusimamia viwanda.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kicheere amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinazalisha Wataalamu bora wa forodha na kodi pamoja na kupanua wigo wa ushirikiano na mataifa ya nje ikiwemo Botswana, Kenya, Burundi na Sudan Kusini.

Amesema  kupitia Chuo hicho mamlaka yake imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inaweza kuzalisha wataalamu wake wa ndani na kupunguza gharama ya kuchukua wataalamu wa nje ya nchi kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali za masuala ya forodha na kodi.

"Lengo letu ni kuhakikisha kuwa ITA kinazalisha wataalamu bora sambamba na kuendelea kuwa  kuwa na Chuo cha Umahiri kama tulivyopendekezwa na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki" amesema Kicheere.

Naye Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Isaya Jairo alisema tangu Chuo kilipopata usajili kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) wameweza kutoa kudahili wanafunzi 6000, ambapo ili kupanua wigo wa masomo ya forodha na kodi, Chuo hicho kimepanga kushirikiana na vyuo mbalimbali vya nje ya nchi.

Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana hadi sasa, Chuo hicho kinaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wanafunzi wengi wa masomo ya shahada kushindwa kuhitimu masomo yao kutokana na ukosefu wa ada.