Chuo chashindwa kudahili wanafunzi

Muktasari:

  •      Baadhi ya watumishi wapelekwa taasisi nyingine za Serikali

 Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius Nyerere (MJNUAT), kilichopo wilayani Butiama Mkoa wa Mara kimeshindwa kudahili wanafunzi kwa zaidi ya miaka mitatu kutokana na ukosefu wa fedha.

Kutokana na hali hiyo, watumishi wa chuo hicho zaidi ya 70 wamekuwa hawana kazi ya kufanya kwa kipindi hicho hali iliyoulazimu uongozi wa chuo kuwapeleka baadhi ya watumishi katika taasisi mbalimbali za Serikali mkoani hapa.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kilichopo Manispaa ya Musoma na shule za sekondari ili waweze kuendelea na kazi wakati taratibu zingine zikifuatwa.

Naibu makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Lesakit Mellau alisema ni vigumu kusema lini chuo hicho kitaanza kudahili wanafunzi kutokana na kutokidhi vigezo vya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU). Profesa Mellau alisema mwaka wa fedha 2014/15 Serikali ilitenga Sh500 milioni kwa ajili ya chuo hicho na mwaka 2015/16 kilitengewa Sh3 bilioni na mwaka 2016/17 kilitengewa Sh10 bilioni fedha ambazo alidai kuwa hazijawahi kupelekwa chuoni hapo.

Hata hivyo, alisema pamoja na ukosefu huo wa fedha, uongozi wa chuo umefanikiwa kufanya mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuandaa sera za chuo, machapisho mbalimbali pamoja na mitalaa ya kuendeshea chuo.

Alisema endapo chuo hicho kitapata fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu na kuajiri watumishi kulingana na ikama ya chuo, upo uwezekano wa kuanza kudahili wanafunzi ambao wataanza masomo yao katika kampasi ya Oswald Mang’ombe.

Oktoba 2016 chuo hicho kilipanga kudahili wanafunzi 2,000 wa masomo ya biashara ambao walitarajiwa kuendelea na masomo yao katika kampasi ya chuo hicho wilayani Bunda lakini mpango huo ulikwama kutokana na ukosefu wa fedha.