Costech yazindua program ya E-Kilimo

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Costech Amos Nungu.

Muktasari:

Programu hiyo  iliyoandaliwa na kusimamiwa na shirika linalojihusisha na masuala ya teknolojia na ujasiriamali (Sahara ventures) itaambatana na mafunzo ya kilimo kwa vijana.

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imezindua programu  maalumu ya kilimo iliyopewa jana la  e-kilimo inayolenga kuongeza kasi  katika ukuaji wa  sekta ya bidhaa za cha kula na mazao nchini.

Programu hiyo  iliyoandaliwa na kusimamiwa na shirika linalojihusisha na masuala ya teknolojia na ujasiriamali (Sahara ventures) itaambatana na mafunzo ya kilimo kwa vijana.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 14, 2018 Kaimu Mkurugenzi Mkuu Costech Amos Nungu  amesema Progamu hiyo imekuja wakati mzuri ambapo Tanzania imezindua mkakati wa pili wa kuboresha kilimo (ASDP)

"Kwa niaba ya Serikali kwa kushirikiana na ubalozi wa Denmark tunataka kuwezesha vijana kushiriki katika maendeleo ya kilimo ambapo watapata fursa ya kujiajiri na kuajiri wengine," amesema na kuongeza kuwa:

"Kutakuwa na maonyesho ambapo siku hiyo vijana watakuja na mawazo mbalimbali ya kibiashara, mawazo ya ubunifu, na mwenye wazo litakaloshinda atapatiwa kiasi cha fedha,".

Mkurugenzi wa shirika la Sahara Ventures Adam Mbyallu amesema mradi huo umegharimu kiasi cha Sh400 milioni.

"Tunaomba vijana wajitokeze kwa wingi katika kushiriki, katika hili tutashirikisha wadau mbalimbali wa kilimo, lakini pia tutapita katika vyuo mbalimbali lengo kupata vijana 200 kwa awamu hii ya kwanza," amesema.