DAS Arumeru ateuliwa kuwania ubunge Korogwe Vijijini kupitia CCM

Muktasari:

  • Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetangaza uchaguzi mdogo katika jimbo hilo utakaofanyika Septemba 16 kutokana na kifo cha Stephen Ngonyani maarufu Profesa Majimarefu aliyekuwa akiliongoza.

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemteua katibu tawala Wilaya ya Arumeru, Timotheo Mzava kuwania ubunge Jimbo la Korogwe Vijijini.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetangaza uchaguzi mdogo katika jimbo hilo utakaofanyika Septemba 16 kutokana na kifo cha Stephen Ngonyani maarufu Profesa Majimarefu aliyekuwa akiliongoza.

Mbali ya kumteua Mzava, Kamati Kuu maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, pia imewateua Julius Kalanga na Mwita Waitara kugombea ubunge katika majimbo Monduli na Ukonga, mtawalia.

Katika kikao kilichofanyika jana ofisi ndogo za CCM jijini Dar es Salaam, Kalanga aliteuliwa kugombea ubunge Monduli ambako alikuwa mbunge kwa tiketi ya Chadema kabla ya kujiuzulu na kuhamia chama hicho sawa na Waitara aliyekuwa Ukonga.

Kamati Kuu kupitia kwa mwenyekiti wake, Rais John Magufuli imewashukuru wananchi waliojitokeza kushiriki katika uchaguzi mdogo wa Jimbo Ia Buyungu na kata 77 na kukipa dhamana chama hicho na wagombea wake kwa kushinda kwa asilimia 100.

CCM katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole imesema kushinda katika uchaguzi ni jambo moja, lakini kuwatumikia wananchi kwa unyenyekevu, uaminifu na kujitoa kushughulika na shida za watu ni jambo jingine.

CCM Arusha

Kabla ya uamuzi huo wa Kamati Kuu Maalumu, mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loata Sanare aliwataka wanachama wa chama hicho walioandamana kupinga Kalanga asigombee wasubiri vikao vya juu vya chama hicho.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano aliouitisha jana kuzungumzia ushindi wa chama hicho katika uchaguzi mdogo wa madiwani, alisema kitendo cha Kalanga kurudi CCM kinaonyesha amejutia makosa yake na sasa ni mwanachama halali wa chama hicho.

“Nafahamu wana CCM walishtuka kusikia mbunge amejiuzulu na kujiunga na chama chetu ikijulikana alikuwa kiongozi kindakindaki wa chama chake, halafu kwa bahati nzuri ndiye pekee aliyejitokeza kuchukua fomu za ubunge kupitia CCM,” alisema Sanare.

Wiki iliyopita, kundi la wanachama wa CCM lilijitokeza hadharani kupinga Kalanga kuteuliwa kuwa mgombea wa chama hicho pasipo kupitia mchakato wa kura ya maoni.

Julai 31, Kalanga alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kurejea CCM, chama alichokuwa amekihama mwaka 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu kufanyika.

Baadhi ya wanachama wa CCM kutoka kata za Isilalei, Monduli Juu na Sepeko waliandamana hadi ofisi za chama hicho wakidai Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson Lengima kwa kushirikiana na viongozi wengine wa chama wanapanga njama ili Kalanga apitishwe kuwa mgombea ubunge pasipo kura ya maoni kufanyika.

Hata hivyo, Lengima alikanusha madai hayo akisema CCM ina utaratibu wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na kuwataka wana-CCM kuwa watulivu.

Katibu wa uenezi wa CCM Kata ya Sepeko, Nooy Naimisye alisema wanataka kuona demokrasia ikitendeka katika kumchagua mgombea ubunge jimboni Monduli.

Nyongeza na Filbert Rweyemamu