DC Hai akana kuibiwa

Muktasari:

Hata hivyo, tukio hilo limegubikwa na utata baada ya mkuu huyo wa wilaya kukana kuibiwa, lakini mlinzi wake ameandikiwa barua ya kujieleza kutokana na tukio hilo.

Hai/Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Gelacius Byakanwa amedaiwa kuibiwa televisheni ya bapa (flat screen) yenye thamani ya Sh1.5 milioni.

Hata hivyo, tukio hilo limegubikwa na utata baada ya mkuu huyo wa wilaya kukana kuibiwa, lakini mlinzi wake ameandikiwa barua ya kujieleza kutokana na tukio hilo.

Byakanwa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, amehoji ni nani aliyeripoti polisi akisisitiza kuwa hakuna tukio kama hilo. “Mimi sina taarifa labda kama OCD (mkuu wa polisi wa wilaya) amekuambia. Nani aliripoti? Mie sina taarifa,”amesema.

Katibu Tawala (Das) wa wilaya hiyo kupitia barua yake ya Oktoba 17, anathibitisha kutokea kwa wizi huo Oktoba 7.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alipotafutwa alisema alikuwa ametingwa na shughuli muhimu na kwamba, akikamilisha atalizungumzia suala hilo.