DC Hapi ampa saa 24 mwenyekiti wa mtaa kujisalimisha

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi 

Muktasari:

Anatuhumiwa kutafuna zaidi ya Sh1 milioni za michango ya wananchi


Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ametoa saa 24 kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Sokoni, Kata ya Tandale, Murshida Diswela kuripoti kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni.

Diswela ambaye ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anadaiwa kukusanya fedha za wananchi zaidi ya Sh1 milioni kwa ajili ya kuzibua mifereji, lakini hadi leo hakuna utekelezaji uliofanyika.

Pia, Hapi amemwagiza ofisa ustawi wa jamii wa kata ya hiyo, Naomi Kasekenya kufanya uhakiki ili kubaini vijana walioandikishwa na kulipwa fedha za miradi ya kusaidia kaya maskini kupitia Tasaf, huku wakiachwa wazee na wenye uhitaji huo.

Hapi ameyasema hayo leo Julai 23, 2018 katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kutembelea kata zote 20 za wilaya hiyo ya jijini Dar es Salaam.

Wananchi wakitoa kero zao kwa Hapi, wamesema Diswela aliwachangisha Sh40,000 kwa kila kaya kwa ajili ya kuzibua mifereji iliyopo eneo hilo, lakini wanapofuatilia hawapewi jibu na mwenyekiti huyo.

"Nakuagiza kamanda wa polisi huyu mwenyekiti kufikia kesho awe amejisalimisha na atoe maelezo yanayojitosheleza fedha za wananchi amezipeleka wapi, hivyo akija na maneno matupu mwekeni ndani," amesema Hapi.

Mkazi wa eneo hilo, Asha Mkunya amesema tangu mwaka 2015 walichangishwa fedha hizo ambapo kwa eneo hilo la Bondeni walitoa Sh400,000 na wanaokaa karibu na sokoni zaidi ya Sh500,000.

Pia amesema fedha za Tasaf baadhi ya viongozi wamekuwa wakigawana wenyewe huku wakiwaandikisha ndugu zao ambao hawastahili kupewa na kuwaacha wazee wenye uhitaji.

Amesema atawaagiza watu kutoka ofisini kwake ili waende kuhakiki kwenye kata hiyo, hivyo watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Ofisa mtendaji wa kata hiyo, Athuman Mtono amesema suala hilo aliligundua wiki iliyopita wakati wakifanya usafi alipelekewa malalamiko kuwa wenyeviti wa serikaki za mitaa wamekuwa wakiingiza watu wao na kuwaacha wazee ambao wanatakiwa kupata fedha za Tasaf.