Thursday, January 12, 2017

DC Kahama aagiza TRA ifuatilie uuzaji wa nyumba

By Shija Felician, Mwananchi sfelician@mwananchi.co.tz

Kahama. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetakiwa kufuatilia mauzo na ununuzi wa nyumba na viwanja katika maeneo mbalimbali wilayani Kahama ili kuwezesha Serikali kukusanya kodi.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Fadhili Nkurklu ambaye pia ameitaka TRA kuanzisha operesheni ya kukagua maduka na maeneo yote ya biashara ili kubaini wasiotumia mashine za kielektroniki za kulipia kodi (EFD).

“Wapo baadhi ya wauzaji na wanunuzi wanaokubaliana kuandika bei ndogo kwenye nyaraka na stakabadhi za mauzo na manunuzi kwa nia ya kukwepa kodi, “ amesema.

Nkurlu amesema watu hao ni lazima wadhibitiwe kwa kufuatilia na kubaini ukweli wa bei halisi.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wanaomiliki maduka mjini Kahama, Shilinde Samandito amesema kila mfanyabiashara anapaswa kutekeleza maelekezo na mahitaji ya kisheria kuhusu kodi na ushuru wa Serikali.

“Chama chetu kimekuwa kikiwahimiza wanachama wake kutumia mashine za EFD na kulipa kodi na ushuru kisheria bila kusubiri kusukumwa na Serikali au TRA,” amesema Samandito.

-->