DC Misungwi avamia sherehe ya ndoa ya mwanafunzi, mkulima

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda .

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda amesambaratisha sherehe ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Igokelo wilayani Misungwi aliyefunga ndoa ya kimila na Masalu Mathayo jana Jumatano Septemba 19, 2018

Mwanza. Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda amesambaratisha sherehe ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Igokelo wilayani Misungwi (jina tunalo) aliyefunga ndoa ya kimila na Masalu Mathayo jana Jumatano Septemba 19, 2018.

Mbali na kusambaratisha ndoa hiyo, baba mzazi wa mwanafunzi huyo na muoaji wamekamatwa na polisi huku maharusi hao wakikimbia kusikojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Septemba 20, 2018 mkuu huyo wa wilaya amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, walifunga safari ya haraka akiambatana na polisi hadi eneo la tukio.

Amesema Mathayo ambaye ni mkulima mkazi wa Igokelo alikuwa tayari ameshafunga ndoa hiyo ikiwa ni baada ya kulipa mahari ya ndama watano.

“Nawahakikishieni kwamba huu mchezo hauwezi kuendelea hapa Misungwi, labda niwe nimehama au vinginevyo. Baadhi ya wazazi na walezi wana hizi tabia za kuwaoza mabinti zao,” amesema Sweda.

Amebainisha kuwa ataendelea kushirikiana na wadau wake wote, wakiwemo watendaji wa kata na vijiji ili kudhibiti tabia na vitendo hivyo ambavyo ni ukiukwaji wa sheria.

“Operesheni tokomeza mimba shuleni ni endelevu na daima adhabu itasalia kuwa kali,” amesema.

Ofisa mtendaji wa kata ya Igokelo, Josephat Mukundi amesema wazazi wamekuwa wakiwaozesha watoto wao kwa kisingizio kuwa watawaachia laana.

“Mzazi unamuamuru binti yake kutofanya vizuri kwenye mtihani wa kitaifa ili afeli na kisha aolewe. Ni visa ambavyo vipo na ushahidi tunao,” amesema Mukundi.