DC Nkulu: Nitashika chaki kufundisha

Muktasari:

Akifungua mafunzo kwa walimu wa halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, moja ya halmashauri zinazounda wilaya ya Kahama, Nkulu amesema uamuzi wake huo unalenga kuhakikisha wanafunzi hawakosi masomo kwa kukosa walimu.

Kahama. Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Fadhili Nkulu ameahidi kuingia darasani kufundisha kukabiliana na uhaba wa walimu wilayani humo.

Akifungua mafunzo kwa walimu wa halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, moja ya halmashauri zinazounda wilaya ya Kahama, Nkulu amesema uamuzi wake huo unalenga kuhakikisha wanafunzi hawakosi masomo kwa kukosa walimu.

Mkuu huyo wa wilaya amewaeleza walimu wanaohudhuria mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia naUfundi kwa uratibu wa Mamlaka ya Elimu nchini (TEA), kuwa atafanya hivyo kwa sababu kitaaluma yeye ni mwalimu.

Mafunzo hayo ya siku tano yanalenga kuwajengea walimu uwezo katika ufundishaji wa masomo ya Hisabati, Kiingereza na Kiswahili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ushetu, Matomola Michael ameahidi kuwa uongozi wa halmashauri utaendelea kushirikiana na wadau wa elimu kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwamo upungufu wa madawati, vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.

Ofisa kutoka ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Jane Nyamsenda aliwataka walimu wanaohudhuria mafunzo hayo kuwa chachu ya mafanikio katika ufundishaji wa masomo ya Hisabati, Kiingereza na Kiswahili katika maeneo yao kwa kuwapa elimu hiyo walimu wengine.