Wananchi wamgomea mkuu wa wilaya

Muktasari:

Mmoja wa wananchi hao, Paulo Simtek amesema  wafugaji wamekuwa wakiishi eneo hilo kwa muda mrefu

Simanjiro. Wananchi wa Kijiji cha Langai, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wamemgomea Mkuu wa wilaya hiyo, Zephania Chaula kugawa ardhi yao wanayodai kuimiliki kihalali.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara jana Machi 18, 2018, wananchi hao wanaojishughulisha na kilimo na ufigaji wamesema hatua hiyo ya mkuu wa wilaya ni ubaguzi.

Mmoja wa wananchi hao, Paulo Simtek amesema  wafugaji wamekuwa wakiishi eneo hilo kwa muda mrefu, lakini kitendo cha mkuu wa wilaya kuchukua mashamba  yao, kuyamega na kuwapatia wakulima kunaweza kuibua migogoro.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Langai, Mathayo Ole Silongoi amesema kuwa  sintofahamu hiyo inatokana na  wa uongozi wa wilaya kudharau Serikali ya kijiji na kufanya uamuzi usiowahusu kwani mashamba hayo yako chini ya Serikali ya kijiji.

Akizungumzia suala hilo, Chaula amesema uongozi wa kijiji hicho umekuwa na ubaguzi wa jamii na ndicho chanzo cha migogoro na kwamba, Serikali itachukua  hatua za kisheria dhidi yao ikiwemo kutoitisha mikutano ya kijiji tangu walipochaguliwa.

"Huo uongozi wa kijiji hatua za kisheria zinawafuata kwa kukiuka  ya uongozi wao waache kusema nimegawa ardhi, bali waseme wao wamefanya nini ikiwemo kuitisha mikutano kusikiliza kero za wananchi na kusoma mapato na matumizi zaidi wanayoyafanya ni kuendekeza ubaguzi wa ukabila," amesema Chaula

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Jakson Siptek amesema wameanza kuchukua hatua za utatuzi na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati hatua zinaendelea.