DC Taka: Ulinzi uimarishwe Ngorongoro kuzuia kupitisha silaha

Muktasari:

  • Akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama kwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Joseph Kakundi juzi, Taka alisema hali ya usalama inaridhisha lakini kuna changamoto ya udhibiti wa silaha za kivita ambayo inatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka.

Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka ameishauri Serikali kupeleka kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wilayani humo ili kuimarisha ulinzi na kuzuia silaha za kivita kuingizwa nchini kupitia njia za panya.

Akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama kwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Joseph Kakundi juzi, Taka alisema hali ya usalama inaridhisha lakini kuna changamoto ya udhibiti wa silaha za kivita ambayo inatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka.

“Wilaya yetu ina eneo la mpaka mrefu na halina udhibiti wa uhakika kwa hiyo, kumekuwa na uingizaji wa silaha unaofanywa na wafanyabiashara wa nchi jirani. Katika operesheni ya hivi karibuni tulikamata bunduki 60 za kivita, tunaamini bado zipo kwasababu zinapatikana kirahisi upande wa pili,” alisema Taka.

Alifafanua kuwa umuhimu wa kuwapo kikosi cha jeshi, utasaidia kulinda eneo la mpaka kuwa salama na kudhibiti vitendo vyenye kuhatarisha amani na utulivu sanjari na kuhakikisha hakuna mtu anayemiliki silaha ya kivita.

Akizungumzia hilo, Kakundi alisema anaunga mkono juhudi za kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuimarisha usalama kutokana na wilaya hiyo kuwa ipo mpakani na nchi jirani na kuendelea kutoa huduma za kijamii kwa wananchi.