DC aamuru mbunge wa Tunduma akamatwe

Mbunge wa Tunduma, wilayani Momba mkoani Songwe, Frank Mwakajoka

Muktasari:

  • Hii ni mara ya pili kwa mbunge huyo kukamatwa baada ya kukamatwa mara ya kwanza Agosti mwaka jana.

Mbeya. Mbunge wa Tunduma, wilayani Momba mkoani Songwe, Frank Mwakajoka amekamatwa na polisi kisha kuwekwa mahabasu kwa saa 48 kwa kile kinachodaiwa ni amri ya mkuu wa wilaya hiyo, Jumaa Irando.

Akizungumza na gazeti hili leo Februari 21, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Mkoa wa Songwe, Ayub Sikagonamo amesema Mwakajoka amekamatwa akiwa kituo cha polisi Tunduma kuitikia wito wa Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo (OCD) baada ya kumpigia simu kwamba anamhitaji ofisini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathias Nyange alisema ‘Nipo nje ya ofisi, in-short’ kisha akakata simu.

Hii ni mara ya pili kwa Mbunge Mwakajoka kukamatwa na kuwekwa mahabusu kwa saa 48 kwa amri ya mkuu huyo wa wilaya. Agosti mwaka jana Irando aliamuru kukamatwa Mwakajoka kwa kile alichodai alitoa lugha ya kumdhalilisha yeye na Serikali ya Mkoa wa Songwe wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara.