DC apiga marufuku walimu kugeuzwa watendaji vijiji, kata

Muktasari:

  • Kipole amesema hatua hiyo ni ili kuwapa muda zaidi wa kutosha kushughulikia maendeleo ya shule zao.

Baada ya mafanikio kwa shule zake kuongeza ufaulu kwenye matokeo ya darasa la saba kwa kushika nafasi ya tatu kimkoa, mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amepiga marufuku walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari kukaimishwa utendaji wa vijiji na kata.

Kipole amesema hatua hiyo ni ili kuwapa muda zaidi wa kutosha kushughulikia maendeleo ya shule zao.

Wilaya ya Sengerema yenye halmashauri za Buchosa na Sengerema ina kata 47 ambazo kati yake 31 ndizo zenye watendaji, huku 16 zinakaimiwa na walimu.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Buchosa imeshika nafasi ya tatu kimkoa huku ikipanda kitaifa kwa nafasi tatu kutoka 28 mwaka 2016 hadi 25. Halmashauri ya Sengerema nayo imepanda kwa nafasi moja kimkoa kwa kushika nafasi ya nne kulinganisha na ya tano iliyoshika 2016. Mwaka huu, halmashauri hiyo imeshika nafasi ya 44 kulinganisha na 52. “Uongozi wa halmashauri zote mbili uangalie namna nyingine ya kuziba nafasi za watendaji wa vijiji na kata zilizopo wazi, walimu waachwe watimize wajibu wao wa kufundisha na kusimamia maendeleo ya elimu,” aliagiza Kipole

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Wilaya ya Sengerema ambayo pia ina majimbo mawili ya uchaguzi ya Sengerema na Buchosa inakadiriwa kuwa na wakazi zaidi 663,034 wanaoishi katika vitongoji 837 vilivyoko ndani ya vijiji 153.

Akizungumzia agizo la mkuu wa wilaya, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda alisema upungufu wa watumishi unaosababishwa na Serikali kusitisha ajira ndio uliowalazimu kukaimisha nafasi za utendaji kwa walimu wakuu.

“Lengo ni kuwezesha wananchi ambao vijiji na kata zao hazina watendaji kuendelea kupata huduma za kusikilizwa kero zao na kuandikiwa barua au kugongewa mihuri kwenye nyaraka mbalimbali,” alisema Luanda.

Kwa mujibu Luanda, kata 11 kati ya 22 za halmashauri hiyo hazina watendaji na hivyo nafasi hizo kukaimiwa na watumishi mbalimbali wakiwamo walimu, huku mkazi wa Kijiji cha Itabagumba, Charles Samson akisema nafasi hizo ni muhimu kujazwa kwa sababu umuhimu wake.