DC asema hataki kutumbuliwa kwa kaya kukosa choo

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa

Muktasari:

Madusa ametoa maagizo  hayo akiwa katika ziara maalumu ya kuhimiza maendeleo na ujenzi wa vyoo kwenye Kata za Chokaa na Sangambi ambako alijionea kaya nyingi zikiwa hazina vyoo.

Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa ametoa  mwezi mmoja kwa kila kaya  isiyo na choo kutozwa faini ya Sh200,000 wilayani humo kwa malengo ya  kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kipindi cha mvua.

Madusa ametoa maagizo  hayo akiwa katika ziara maalumu ya kuhimiza maendeleo na ujenzi wa vyoo kwenye Kata za Chokaa na Sangambi ambako alijionea kaya nyingi zikiwa hazina vyoo.

Akizungumza leo (Jumatano) amesema hatakubali ugonjwa wa kipindupindu uwe chanzo cha yeye kutumbuliwa  kwenye wadhifa wake na kwamba lazima kila kaya iwe na choo safi ili kuepuka kusambaa kwa uchafu wakati wa mvua.

Kauli hiyo anaitoa huku kukiwa na agizo la Rais John Magufuli alilolitoa kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama bila kipindupindu kuepuka kutumbuliwa.