DC atimuliwa kazi akiwa ziarani na waziri mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulru wakati alipowasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama  kuzungumza na watumishi wa Umma, mkoani Shinyanga jana. Mkuu huyo wa wilaya alitenguliwa wadhifa huo na Rais John Magufuli muda mchache baada ya tukio hilo. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu imeeleza kuwa badala yake, Rais Magufuli amemteua Anamringi Macha kujaza nafasi hiyo akitakiwa kuripiti katika kituo chake cha kazi mara moja.

Kahama. Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu kuanzia jana.

Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu imeeleza kuwa badala yake, Rais Magufuli amemteua Anamringi Macha kujaza nafasi hiyo akitakiwa kuripiti katika kituo chake cha kazi mara moja.

Nkurlu alitimuliwa kazi akiwa katika msafara wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wilayani hapo. Saa chache kabla ya taarifa hiyo ya Ikulu, Majaliwa alikemea kuhusu migogoro ya kiuongozi wilayani hapa akisema watumishi wa umma wanapaswa kubadilika mara moja.

Akizungumza na watumishi hao na viongozi wa halmashauri za wilaya za Ushetu, Msalala na Kahama Mji, alisema, “Migogoro niliyoisikia ambayo iko hapa ni kwa sababu ninyi mmeingia kwenye biashara na kutake sides (kuwa na upande). Hapa Kahama, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa wilaya hamuelewani, mkurugenzi na wakuu wa idara hamuelewani, wakuu wa idara na wasaidizi wao nao pia hawaelewani.”

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana imeongeza, “Hali ya mahusiano hapa Kahama ni mbaya kuliko Kishapu na Shinyanga. Mnachapa kazi vizuri lakini tatizo kubwa kila mmoja anaenda kivyake, hakuna anayemsikiliza mkurugenzi wa halmashauri wala mkuu wake wa idara.

“Serikali haitavumilia kuona watumishi wakifanya mambo ya ovyo. Kahama ni wilaya yenye majaribu na Shinyanga nayo ni wilaya yenye majaribu makubwa. Kwa hiyo watumishi inabidi muwe makini, kuweni waangalifu msije mkaingia kichwakichwa kwenye majaribu haya.”

Alisema Kahama ina fursa kubwa na nzuri kwenye kilimo, madini, mifugo na biashara, hivyo akawataka viongozi wanaopelekwa kwenye wilaya hiyo wawe makini.

“Kiongozi ukiletwa hapa inabidi uwe na kichwa kilichotulia. Inabidi uwe mwaminifu sana ili uweze kudumu kwenye wilaya kama hii. Kama kiongozi ulizoea kwenda disko inabidi uache, kama ulizoea kwenda baa inabidi ununue kreti uweke ndani kwako. Kama ulizoea kushabikia mpira kwa kujichora chaki, sasa basi. Kaa sebuleni kwako, angalia mpira kwenye luninga yako, ndiyo dhamana ya uongozi hiyo,” alisema.

DC alivyopata taarifa

Saa chache kabla ya uteuzi wake kutenguliwa, Nkurlu alishiriki kikamilifu katika ziara hiyo ya Waziri Mkuu tangu asubuhi wakati wa kikao cha watumishi wa halmashauri zote tatu za Kahama Mji, Msalala na Ushetu na akiwa katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji alisoma taarifa ya wilaya. Akiwa mwenyeji, alimwongoza Waziri Mkuu kutembelea Kituo cha Afya Mwendakulima na kiwanda cha Kahama Oil Mill.

Wakiwa katika eneo la viwanda wa mbao saa 9:26 alasiri ndipo taarifa za kutenguliwa kwake zilipoanza kusikika na na mara moja alitoweka kwenye msafara huo.

Baada ya msafara huo kufika kwenye mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji, mshehereshaji Nyanzala Kalegea alimwita kwa jina mkuu huyo wa wilaya ili kutambulisha wageni lakini hakutokea. Baadala yake katibu tawala wa wilaya hiyo, Timothy Ndanya alisimama na kwenda kwenye kipaza sauti na kufanya kazi hiyo ambayo tangu asubuhi ilikuwa ikifanywa na Nkurlu.