DC awakomalia watu waliojenga mabondeni

Zanzibar. Licha ya Wilaya ya Magharibi A kufanya juhudi za kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia taratibu za ujenzi, elimu hiyo inaonekana kugonga mwamba.

Wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, wamebainika kuanzisha ujenzi wa majengo mapya maeneo hatarishi (mabondeni na vianzio vya maji).

Ujenzi huo unafanyika bila vibali vya ujenzi kutoka halmashauri ya wilaya hiyo au mipango miji.

Akiwa katika ziara ya kutembelea maeneo ya Msikiti Mzuri na Misufini katika shehia ya Mwera kuangalia changamoto za ujenzi, Mkuu wa Wilaya Magharibi A, Khatib Khamis alisema mbali na juhudi zinazochukuliwa kukomesha hali hilo, wananchi wameendelea kutotii agizo hilo.

Khatib alisema licha ya kutoa elimu kwa wananchi kupitia masheha wao juu ya umuhimu wa kuzingatia taratibu za ujenzi, ikiwamo upatikanaji wa vibali, watu wengi wamekuwa wakipuuza agizo hilo.

Alisema kabla ofisi yake ilisimamisha ujenzi katika majengo yaliobainika kwenda kinyume na taratibu hizo, sambamba na kuwataka wamiliki wake kuripoti ofisini kwake wakiwa na uthibitisho ulioidhinisha ujenzi huo, lakini wengi wa wamiliki wa majengo hayo wamekuwa wakipuuza maagizo hayo.

Pia, alisema mbali na hatua hiyo kuiweka jamii katika mazingira hatarishi, lakini kwa kiwango kikubwa inaikosesha mapato Serikali.

Khamis alitoa siku tano kwa wamiliki wa majengo yote waliyafanyia ukaguzi kufika ofisini kwake wakiwa na vibali vya ujenzi, kwa watakaoshindwa kufanya hivyo majengo yao yatakuwa chini ya dhamana za masheha.

Alisema yaliyokosa vibali wataangalia uwezekano wa kuyatumia kwa shughuli za kijamii, ikiwamo uanzishaji vituo vya afya.

Baadhi ya wamilliki wa nyumba hizo waliiomba Serikali kuwasemehe kutoka na maeneo hayo waliuziwa zamani bila kujua kuwa hairuhusiwi.

zisizoruhusiwa kisheria.