VIDEO: Dada wa Rais Magufuli afariki dunia

Muktasari:

Ni siku moja kupita tangu alipomtembelea hospitalini

Dar es Salaam. Dada wa Rais John Magufuli, Monica aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza amefariki dunia leo Augusti 19, 2018.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa kupitia akaunti zake za kijamii ameandika ujumbe ukiambatana na picha ya dada huyo wa Rais Magufuli akisema;

“Nasikitika kuwajulisha kuwa Dada wa Rais (John Magufuli) Monica Joseph Magufuli amefariki dunia asubuhi leo Agosti 19, 2018 katika hospitali ya Bugando jijini Mwanza alikokuwa akipatiwa matibabu,” amesema Msigwa.

“Natoa pole kwa Rais John Pombe Joseph Magufuli, familia ya Mzee Joseph Magufuli, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu,” ameongeza.

Msigwa amemaliza kuandika ujumbe wake akisema, “Raha ya milele umpe e Bwana na mwanga wa milele umuangazie, marehemu Monica Jospeh Magufuli astarehe kwa amani, Amina.”

Jana, Rais Magufuli alifika hospitalini hapo kumjulia hali dada yake.