Daktari aeleza hali ilivyokuwa alipokwenda kumtibu Kanumba

Muktasari:

Daktari amesema alipompima Kanumba kiwango cha sukari kilikuwa cha kawaida lakini alipompima shinikizo la damu hakupata kabisa mapigo ya moyo.

Dar es Salaam. Daktari Paplas Kagaiya aliyekuwa akimtibu msanii maarufu wa fani ya uigizaji filamu nchini, Steven Kanumba ametoa ushahidi Mahakama Kuu akieleza hali aliyoikuta alipokwenda nyumbani kwa msanii huyo.

Mbali na Dk Kagaiya, askari Polisi aliyemtia mbaroni msanii wa kike Elizabeth Michael, maarufu Lulu, pia ametoa ushahidi mahakamani hapo leo Ijumaa Oktoba 20,2017.

Lulu ambaye yuko nje kwa dhamana anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia kosa analodaiwa kulitenda  Aprili 7,2012, Sinza Vatican jijini Dar es Salaam nyumbani kwa Kanumba.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Batilda Mushi kutoa ushahidi, Dk Kagaiya amesema alipofika nyumbani kwa Kanumba alikuta akiwa ameanguka na alimpima kiwango cha sukari na shinikizo la damu.

Amesema kiwango cha sukari kilikuwa cha kawaida lakini alipompima shinikizo la damu hakupata kabisa mapigo ya moyo, hivyo alishauri Kanumba apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dk Kagaiya amesema daktari katika kitengo cha dharura Muhimbili alipompima Kanumba aliwaeleza alikuwa tayari ameshafariki dunia.

Baada ya kupewa maelezo hayo, amesema walikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Selander Bridge.

Shahidi huyo alipoulizwa na wakili wa Lulu, Peter Kibatala kama kuna vitu vyovyote alivyoviona eneo la tukio chumbani kwa Kanumba, ikiwemo chupa ya pombe alisema hakutambua chochote.

Katika hatua nyingine, askari Ester Zefania kutoka Kituo cha Polisi Msimbazi akitoa ushahidi amesema alikwenda kumkamata Lulu alfajiri, eneo la Bamaga kwa msaada wa Dk Kagaiya, ambaye walikuwa wakiwasiliana kwa simu.

Akijibu swali la wakili Kibatala kama alimpeleka Lulu hospitalini kwa matibabu, shahidi huyo amesema ni kweli alimpeleka hospitali.

Hata hivyo, Zefania amesema Lulu hakumueleza kuwa alipigwa na Kanumba na wala hakuona majeraha. Alijibu hayo baada ya kuulizwa swali na wakili Kibatala.

Zefania amesema aliagizwa na mkuu wake wa kazi ampeleke Lulu hospitalini lakini hakujua alikuwa ana matatizo gani.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Sam Rumanyika itaendelea Jumatatu Oktoba 23,2017 kwa upande wa mashtaka kukamilisha ushahidi wake.