Daktari akwamisha kesi ya mwalimu anayetumiwa kumbaka mwanafunzi

Muktasari:

  • Kesi inayomkabili mwalimu wa shule ya sekondari ya Adili ya jijini Arusha, Joel Mbaga akituhumiwa kumlawiti mwanafunzi wake wa kiume (13) wa kidato cha kwanza imekwama kuendelea kutokana na shahidi wa nne kutofika mahakamani .

Arusha. Daktari wa hospitali ya mkoa ya Mount Meru, ambaye ni shahidi wa nne, katika kesi ya kumlawiti mwanafunzi wa kiume wa kidato cha kwanza wa shule ya Sekondari Adili ya Arusha, inayomkabili mwalimu wa shule hiyo, Joel Mbaga (27), ameshindwa kufika mahakamani kwa mara ya tatu.

Shahidi huyo (jina linahifadhi), ambaye ni daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo, imeelezwa na mwendesha mashitaka wa Serikali, Naomi Mollel  ameshindwa kutokea mahakamani  kutokana na kukabiliwa na dharura.

Hakimu mkazi Patricia Kisinda baada ya kupokea taarifa ya mwendesha mashitaka huyo leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 wa Serikali iliahirisha kesi hadi Oktoba 28 na kuutaka upande wa Jamhuri kuhakikisha unamfikisha mahakamani shahidi huyo.

Katika kesi hiyo namba 165 ya mwaka 2018, Mwalimu Mbaga anatuhumiwa kutenda kosa hilo kati ya Septemba na Oktoba, 2017 wakati akijua ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, mwalimu huyo amekuwa akikanusha tuhuma hizo na kueleza mtoto huyo, aliingiliwa na popobawa kutokana na barua aliyoandika kwa uongozi wa shule hiyo kugoma kurejea shule. Mwalimu huyo yupo nje kwa dhamana.

Katika kesi hiyo, tayari mashahidi watatu wametoa ushahidi wao ambao ni mwanafunzi aliyefanyiwa uhalifu, mama mzazi wa mtoto huyo, Agness Augostino na mwalimu mwingine wa shule hiyo, Florian Masawe.