Wataalamu wataja sababu Dar kuwa na wagonjwa wengi wa TB

Muktasari:

Mkoa unaofuatia kwa kuwa na wagonjwa wengi ni Mwanza kwa asilimia (6), Mbeya (5), Arusha (5), Dodoma (5) na Morogoro (5).


Dar es Salaam.  Takwimu mpya za mwaka 2017, zimebaini kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia 20 ya wagonjwa wa Kifua Kikuu (TB), idadi inayotajwa kuwa ni kubwa ukilinganisha na mikoa mingine.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 24 katika mkutano wa vyombo vya habari, kuhusu ufuatiliaji wa tathmini kutoka mpango wa taifa wa kudhibiti TB nchini.

Mkoa unaofuatia kwa kuwa na wagonjwa wengi ni Mwanza kwa asilimia (6), Mbeya (5), Arusha (5), Dodoma (5), Morogoro (5) na mikoa iliyosalia ilijumuisha katika asilimia 54 zilizosalia. 

Mfuatiliaji wa Tathmini kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti TB, Dk Zuweina Kondo amesema wingi wa wagonjwa hao kupatikana Dar es Salaam imechangiwa na uwapo wa vituo vingi vya maabara vinavyopima vimelea vya ugonjwa huo. 

"Mkoa huu una idadi kubwa ya wagonjwa tuliowagundua na kuwaweka katika matibabu, hii haimaanishi kuwa ndiyo unaoongoza Tanzania, hapana. Ila, ni mkoa wenye maabara nyingi ambazo zinaweza kuhudumia jamii kwa upana wake," amesema.

Dk Kondo amesema takwimu hizo nchini zinaonyesha watu 287 kati ya 100,000 wana maambukizi ya vimelea vya ugonjwa wa TB.

Ripoti ya NBS ya mwaka 2018 ya idadi ya watu milioni 54, takwimu zinaonyesha kati yao 160,000 wanaugua ugonjwa huo kati ya Watanzania wote.

Hata hivyo, Dk Kondo amesema baada ya vipimo vya maabara  nchini wameweza kuwabaini Watanzania 64,000 na kuwaingiza kwenye dawa sawa na asilimia 40 ya waliotarajiwa kufikiwa, huku asilimia 60 wakishindwa kuwapata.

Naye naibu meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk Liberate Mleoh amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 zenye maambukizi makubwa duniani.

 Kuhusu TB

*Ni ugonjwa sugu unaoambukizwa na vimelea aina ya bakteria visivyoonekana kwa macho ila kwa hadubini. Kuna kifua kikuu cha ndani ya mapafu na nje ya mapafu. 

*Watu zaidi ya bilioni mbili duniani wanaugua TB na ni ugonjwa unaoshika nafasi ya tisa kwa kuua kati ya magonjwa yanayosababishwa na vimelea.

*Kila mwaka husababisha vifo milioni 1.3 kwa wasio na virusi vya Ukimwi (VVU) na vifo 374,000 kwa waliokuwa na VV