Dawasa yadaiwa ada ya maji

Muktasari:

Bodi hiyo inashindwa kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji kutokana na kuwepo wateja wengi wanaodaiwa ada kutumia maji hayo.

Dar es Salaam. Bodi ya Maji, Bonde la Wami/Ruvu imewataka watumiaji wa maji wakiwemo mamlaka za usambazaji maji kulipa ada za matumizi ya maji ili kuwezesha bodi hiyo kufanya shughuli zake kwa ufanisi.

Bodi hiyo imedai kuwepo kwa idadi kubwa ya watumiaji wa maji wanaolimbikiza ada za matumizi ya maji na kuifanya ishindwe kutekeleza jukumu lake la kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji ikiwemo mito.

Wadaiwa sugu hao ni pamoja na wamiliki wa visima majumbani na Mamlaka ya maji safi jijini Dar es Salaam (Dawasa) ambayo inadaiwa zaidi ya Sh1 bilioni.

Ofisa wa Maji wa bonde hilo, Simon Ngonyani akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 19, 2018 amesema bodi hiyo inashindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya kukosa fedha.

Kufuatia hilo bodi imetoa mwezi mmoja kwa wadaiwa wote kulipa madeni yao kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa.

Kwa upande wa Dawasa, Ngonyani amesema deni hilo limekuwepo kwa muda wa miaka minne sasa lakini tayari ameshazungumza na mkurugenzi wa fedha wa mamlaka hiyo ambaye ameahidi kulifanyia kazi hivi karibuni.

"Labda niwakumbushe kwamba wao jukumu lao ni kusambaza na sisi tunataka kufanya kazi yetu, jana nilikutana na uongozi wao tumekubalina kwamba watalipa,"

"Maji hayawezi kufika kwa watumiaji kama kule juu kwenye vyanzo hayakutunzwa na kuhifadhiwa vizuri. Watu wanadhani maji ni mabomba, hapana yanaanzia kule kwenye vyanzo," amesema.