Dege la Emirates na abiria wake 475, latua Dar kwa dharura

Muktasari:

  • Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 475, inatajwa kuwa ni ya kwanza yenye ukubwa huo kutua katika uwanja wa ndege wa Tanzania.

Ndege kubwa ya aina yake, Airbus 380, EK701 ya Shirika la Ndege la Emirates iliyokuwa ikielekea Mauritius imetua kwa dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, (JNIA) kutokana na hali mbaya ya hewa nchini humo.

Ndege hiyo iliyokuwa na abiria 475, inatajwa kuwa ni ya kwanza yenye ukubwa huo kutua katika uwanja wa ndege wa Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema ni mara ya kwanza kwa ndege yenye ukubwa huo aina ya ‘Airbus’ kutua katika ardhi ya Tanzania.

Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi Matanga Mbushi amesema ndege hiyo ilishindwa kutua mara tatu nchini Mauritius kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.

“Hiyo ndege ilikuwa ikielekea Mauritius, sasa hali ya hewa imekuwa mbaya ikashindwa kutua. Rubani alijaribu kutua mara tatu lakini akashindwa ndipo akaamua kuja Dar es Salaam kutua kwa dharura,” alisema Mbushi.

Alisema ndege hiyo ilikuwa na abiria 475 na wote wamepangiwa hoteli ili kusubiri taarifa za hali ya hewa ikiwa nzuri waendelee na safari.

“Kesho (leo) kama hali itakuwa nzuri wataondoka,” alisema Mbushi.

Ndege hiyo ni ya Shirika la Emirates la Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Ni kampuni tanzu ya Emirates Group ambayo inamilikiwa na Shirika la Uwekezaji la Serikali ya Dubai.

Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ali Mtanda amekanusha madai ya kusumbuliwa kwa abiria wa ndege hiyo akisema wanachotakiwa ni kulipia viza ya mpito.

“Hizo habari siyo za kweli kwasababu hilo suala limetokea kwa dharura na inakubalika kimataifa kwa hiyo hatuwezi kuwasumbua,” alisema Mtanda.

“Wanachotakiwa ni kulipa ‘transit visas’, siwezi kujua kiwango kwa sababu sijui wanatoka nchi gani,” aliongeza Mtanda.

Taarifa zinasema ndege hiyo ni kubwa kuliko zote zilizowahi kutua katika uwanja huo.