Republican yaanguka uchaguzi Alabama

Muktasari:

Doug Jones wa Democratic amembwaga mpinzani wake Roy Moore wa Republican.

Alabama, Marekani. Mgombea wa Democratic katika uchaguzi maalumu kujaza nafasi kwenye Baraza la Seneti nchini Marekani, Doug Jones ameibuka mshindi.

Jones amembwaga mpinzani wake Roy Moore wa chama cha Republican.

Mshindi huyo atakayeapishwa mwezi ujao ataliwakilisha Jimbo la Alabama lililoko kusini mwa Marekani.

Kwa matokeo hayo, wingi wa Republican katika Baraza la Senati utapungua na kuwa na viti 51 dhidi ya 49 vya Democratic.

Kupungua kwa kiti hicho kutaongeza ugumu kwa Rais Donald Trump kupitisha ajenda zake.

Muda wa kuhudumu katika Baraza la Seneti ni miaka sita lakini Jones anajaza nafasi kwa muda uliobaki wa miaka mitatu.

Kiti hicho awali kilikuwa kikishikiliwa na Jeff Sessions ambaye alijiuzulu ili kuwa mwanasheria mkuu katika utawala wa Trump.

Jones ni mwanachama wa kwanza wa Democratic kutoka Alabama kushinda kiti cha seneti tangu mwaka 1992.

Moore alikuwa akiungwa mkono na Trump lakini alikabiliwa na upinzani kutoka kwa viongozi wengine wa Republican.