Deni la Taifa sasa ni Sh47.7 trilioni

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango 

Muktasari:

  • Deni la nje ni Sh34.148 trilioni sawa na asilimia 71.5, deni la ndani lilikuwa Sh13.607 trilioni sawa na asilimia 28.5.


Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema hadi Desemba 2017, deni la Taifa lilikuwa limefikia Sh47.756 trilioni na tathmini zinaonyesha bado ni himilivu.

Akiwasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19 mjini hapa leo Machi 13, 2018, Dk Mpango amesema deni la nje lilikuwa  Sh34.148 trilioni sawa na asilimia 71.5 na deni la ndani ni Sh13.607 trilioni sawa na asilimia 28.5.

Hata hivyo amesema uwiano wa deni hilo na Pato la Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo ambao ni asilimia 56.

“Uwiano wa deni la nje na mauzo ya nje ni asilimia 81.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150. Hii inamaanisha kuwa uwezo wetu wa kulipa deni bado ni imara,” amesema.

Amesema Serikali inaendelea kuchukua tahadhari kwa kukopa kwenye vyanzo vyenye masharti nafuu kuhakikisha mikopo hiyo inaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.