VIDEO: Dereva, utingo wasimulia kilichotokea ajali iliyoua watu 15

Muktasari:

Juzi, magari matano likiwamo lori la mafuta, basi dogo na magari mengine matatu yaligongana na kusababisha vifo hivyo.

Mbeya. Siku mbili baada ya watu 15 kufariki dunia katika ajali iliyotokea juzi na kuhusisha magari matano katika mteremko wa Mlima Igawilo mkoani Mbeya, dereva na utingo walionusurika ajalini wameeleza jinsi tukio hilo lilivyotokea.

Juzi, magari matano likiwamo lori la mafuta, basi dogo na magari mengine matatu yaligongana na kusababisha vifo hivyo.

Wakizungumza wakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, majeruhi hao walisema kunusurika kwao kulitokana na bahati ya aina yake.

Ajali hiyo ilisababishwa na lori kufeli breki likiwa katika mteremko huo na kuyagonga magari mengine manne yaliyokuwa mbele.

Kondakta wa daladala lililogongwa na lori hilo, Semeni Zalanga alisema ajali hiyo ilitokea wakiwa katika Kituo cha Mabasi cha Ntozo wakibeba na kushusha abiria, ndipo lori lililokuwa limepakia viazi lilipowagonga kwa nyuma.

“Tulipomaliza kupakia abiria kabla hatujaondoka lori hilo lilikuja kasi kwa nyuma ndipo likatugonga kisha likatuburuza kwa umbali kidogo huku likiwa juu ya gari letu, hivyo tukaburuzwa na baada ya hapo sikujua kilichoendelea na nikajikuta nipo hospitali na hali hii,” alisema kondakta huyo.

Dereva wa kampuni ya Asas ambaye gari analilokuwa akiendesha nalo lilihusika katika ajali hiyo, Saku Mohamed alisema alikuwa mbele ya daladala hilo.

“Nilikuwa mbele ya daladala na lori hilo, hivyo baada ya daladala hilo kugongwa na kuburuzwa kabla ya kwenda kwenye mtaro lori lile lilikuja kasi na kugonga gari langu na likatupwa nje ya barabara,” alisema Mohamed.

Alisema kwa kuwa lori hilo lilipoteza mwelekeo liliyagonga magari mengine ya mbele na kisha kuacha njia na kuwaka moto.

“Lakini nashukuru wasamaria wema walinitoa katika gari na kunileta hospitalini hapa. Kwa sasa najisikia maumivu kwenye mkono na sehemu ya nyoga ila madaktari wanajitahidi kadri ya uwezo wao kutoa huduma.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema magari yote yalikuwa yakitokea barabara ya Tukuyu kwenda jijini Mbeya na yalipofika eneo hilo, lori lililokuwa limebeba viazi lilifeli breki kisha kuigonga daladala na kuiburuza.

Baada ya daladala kutupwa kwenye mtaro, lori hilo liliendelea kuyagonga magari mengine na baadaye likawaka moto.

Matei alisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo halisi licha ya eneo hilo kuwa hatari kutokana na uwepo wa mlima mkali na wembamba wa barabara.

Muuguzi mkuu

Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Petro Seme alisema juzi walipokea majeruhi 15 na miili ya watu 13 ambao walipoteza maisha eneo la tukio.

“Lakini wawili kati ya majeruhi hao walifariki wakati wakiendelea kupatiwa matibabu na majeruhi wanne walitibiwa na kuruhusiwa ila wengine wanaendelea na matibabu,” alisema Dk Seme.

Alisema, “majeruhi waliopo kwa sasa ni tisa, ila wawili wapo chumba maalumu cha uangalizi (ICU) na mmoja hali yake si nzuri. Wengi wao wameumia zaidi kichwani, kuvunjika miguu na mikono na tunaendelea na matibabu.”

DC, mbunge watua

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika alifika jana asubuhi kuwajulia hali majeruhi hospitalini hapo na kuwatakia uponaji wa haraka. “Tunawapa pole ndugu zetu waliopoteza maisha, ni jambo la huzuni lakini tuendelee kuwatia moyo wenzetu ambao ni majeruhi wakiendelea na matibabu ili waweze kurejea kwenye majukumu yao ya kila siku,” alisema

Naye mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alifika na kuwapa pole majeruhi, ndugu na jamaa waliopoteza wapendwa wao, na pia kutoa ushauri ulioambatana na ujumbe kwa viongozi wa Serikali.

Aliwataka viongozi kuacha kuchukua hatua kwa mihemko ya kisiasa badala ya kuangalia uhalisia wenyewe.

“Ajali zinamaliza nguvu ya familia, jamii ya eneo husika na Taifa kwa ujumla, lakini upo uwezekano mkubwa wa kumaliza tatizo, hivyo Serikali na wadau wengine wanatakiwa kukaa kitaalamu kuona namna bora ya kuziepusha,” alisema.

Sugu alisema ajali hizo zina uhusiano mkubwa na jiografia ya mkoa huo kutokana na mazingira yenye milima na miteremko.