Dereva aliyeteketea kwa moto Rusumo atambulika

Muktasari:

Ni mkazi wa Dar es Salaama kama ilivyo kwa utingo aliyejeruhiwa katika ajali hiyo iliyosababishwa na lori kufeli breki na kugonga magari mengine saba

Ngara. Dereva aliyeteketea kwa moto katika ajali ya gari katika kituo cha forodha Rusumo wilaya ya Ngara mkoani Kagera mpakani mwa Tanzania na Rwanda ametambulika kuwa ni Abdalah Salimu (37) mkazi wa Dar es Salaam.

Pia, utingo aliyejeruhiwa ni Hajji Mohammed (22) naye mkazi wa Dar es Salaam baada ya gari aina ya scania mali ya kampuni ya Lake Oil kufeli breki na kugonga magari mengine saba yaliyosababisha kuteketea kwa moto pamoja na trekta moja leo asubuhi.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Agustino Olomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Amesema magari ya zimamoto kutoka Karagwe yalifika na kusaidiana na helikopta ya kijeshi ya Rwanda ikionyesha mahusiano ya ujirani mwema na kwamba shughuli za wananchi zimerejea kama kawaida.

"Juhudi zilizofanywa na kikosi cha zimamoto Karagwe na wenzetu kutoka Rwanda zimesaidia kwa haraka kuepusha madhara zaidi kwani ungeweza kusambaratisha hata nyumba kama moto ungezigusa nyaya za umeme" Amesema Olomi

Naye mkuu wa mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewashukuru viongozi wa Serikali ya Rwanda walioungana kutoa helikopta kuzima moto huo wakiwa  na kikosi cha zimamoto kutoka wilayani Karagwe.

Kesho mkuu huyo wa mkoa atakuwa na ziara ya siku moja wilayani Ngara kujitambulisha kwa wananchi na watendaji wa Serikali baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli hivi karibuni kuchukua nafasi ya Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu aliyestaafu.