VIDEO-Dereva atimua mbio, wahamiaji 83 wadakwa

Muktasari:

Mtuhumiwa awaruka, adai alipewa lifti kutoka Dar, akadakwa akifanya usafi

Zikiwa zimepita siku tatu tangu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam iwahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela wahamiaji haramu 77 kutoka Ethiopia, wengine 83 wamedakwa mkoani Iringa huku dereva aliyekuwa akiwasafirisha akifanikiwa kutoroka.

Wahamiaji hao walikamatwa wilayani Kilolo mkoani hapa wakiwa safarini kupelekwa Malawi kisha Afrika Kusini.

Hata hivyo katika harakati za kukamatwa kwao, dereva wa lori mali ya mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya alitoroka.

Raia hao wa Ethiopia walikamatiwa katika Kijiji cha Mbigili ambapo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Iringa, Hope Kawawa alisema walikamatwa juzi saa kumi na moja jioni karibu na bomba la mafuta la Tazama.

Alisema wahamiaji hao walipelekwa kituo cha polisi cha Lugalo na kwamba, kukamatwa kwao kunatokana na taarifa iliyofikishwa Uhamiaji na wananchi.

Alisema maofisa wa Uhamiaji kwa kushirikiana na polisi walipowakamata baadhi yao waliwakuta hali zao ni mbaya kutokana na kukosa chakula kwa siku tatu na pia kuathiriwa na joto kutokana na bodi la lori walilokuwa wakisafiria kuwa la bati. “Wahamiaji hawa walikuwa wanasafiri kwenye lori mali ya mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya, dereva alikimbia na hajapatikana lakini uchunguzi unaendelea,” alisema.

Aliongeza kuwa wahamiaji hao watafikishwa mahakamani kesho kujibu mashtaka yanayowakabili.

“Naomba niwaambie madalali wanaosafirisha hawa wahamiaji kuwa mkoa wa Iringa si mahala salama kuwapitisha kwa kuwa tuko makini saa 24 na tukiwabaini hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa pindi wanapohisi baadhi ya watu si raia wa Tanzania na wanapowaona watu wasiowatambua. Mtanzania aliyekamatwa akihusishwa na usafirishaji wa wahamiaji hao, Hassan Mwalusanjo alisema hana anachofahamu.

Alisema aliomba lifti katika gari hilo kutoka Tukuyu kwenda Dar es Salaam kununua vifaa vya gari wakati gari hilo lilipokuwa likisafirisha ndizi. Mwalusajo alisema baada ya kushusha ndizi eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam, dereva aliondoka na aliporeja alipanda kurejea Tukuyu.

Alisema walipofika Ilula alishuka kula ndipo dereva alipoondoka na gari na aliporejea alimuomba amsaidie kusafisha gari.

“Sielewi chochote nilishangaa kuwekwa chini ya ulinzi baada ya dereva kuniambia nimsaidie kusafisha gari ambako nilikuta makopo ya maji na mifuko ya mikate,” alisema akiwa chini ya ulinzi.’’