Dhoruba baharini yaondoka na maisha ya watu 12

Muktasari:

Wakulyamba amesema katika tukio hilo watu wengine 34 wameokolewa kufuatia mashua hiyo kupigwa na dhoruba na kuzama  Bahari ya Hindi.

Tanga. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,  Benedict Wakulyamba amesema watu 12 wamekufa baada ya mashua iliyokuwa ikienda Pemba kuzama.

Wakulyamba amesema katika tukio hilo watu wengine 34 wameokolewa kufuatia mashua hiyo kupigwa na dhoruba na kuzama  Bahari ya Hindi.

Watu hao wameokolewa na kikosi cha wavuvi waliokuwa baharini eneo la Jambe ambalo ni jirani na pwani ya Mkoa wa Tanga.

Abiria walionusurika katika ajali hiyo wamesema mashua hiyo iling’oa nanga Bandari ya Sahare jijini Tanga ikiwa na abiria 52 pamoja na shehena ya mizigo kama mifuko ya mchele, pumba, viazi maharage na masanduku ya bia.

Wamesema baada ya kufika eneo la Jambe, mashua hiyo ilipigwa na dhoruba upande wa nyuma ikapoteza mwelekeo na kwa kuwa kulikuwa na upepo mkali abiria walianza kuzama baharini.

Mmoja wa abiria wa mashua hiyo, Mkubwa Yussuph Hassan (55) amesema sababu kubwa ya kuzama ni mashua hiyo ni kutoboka chini na hivyo kuruhusu maji kuingia kwa kasi.

“Ndiyo maana hata hatukuweza kuwapigia simu jamaa zetu wa Pemba na Tanga kwa sababu kitendo cha kupigwa na dhoruba na kujaa maji kilikuwa cha haraka. Hata simu zetu zililowana,”amesema Mkubwa Yussuph Mbwana ambaye ni mzaliwa wa Pemba na mkazi wa Mtaa wa Nguvumali jijini Tanga.

Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) mkoani Tanga, Dk Walukani Luhamba amesema ajali hiyo ni matokeo ya manahodha kupuuza maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa juu ya kufuata sheria na taratibu za usafiri wa majini.